Anayedaiwa kumteka Mo Dewji ahoji upelelezi kesi inayomkabili

Muktasari:

Upande wa utetezi kesi ya kutekwa mfanyabiashara Mohammed Dewji ‘Mo’ inayomkabili dereva teksi, Mousa Twaleb umeutaka upande wa mashtaka kueleza ulipofikia upelelezi wa shauri hilo.

Dar es Salaam. Upande wa utetezi kesi ya kutekwa mfanyabiashara Mohammed Dewji ‘Mo’ inayomkabili dereva teksi, Mousa Twaleb umeutaka upande wa mashtaka kueleza ulipofikia upelelezi wa shauri hilo.

Twaleb ambaye ni mkazi wa Tegeta  na wenzake wanakabiliwa na mashtaka matatu katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 42/2019.

Hayo yamelezwa leo Jumanne Novemba 12, 2019 na wakili wa utetezi, Mahfudhu Mbagwa katika  mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu lilipotajwa shauri hilo.

Mbagwa ametoa maelezo hayo baada ya wakili wa Serikali, Glory Mwenda kuieleza mahakama hiyo kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na kuomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.

Maelezo ya Mwenda yalimfanya Mbagwa kudai mteja wake anaendelea kukaa rumande kwa muda mrefu kutokana na upelelezi kutokukamilika kwa wakati.

Akijibu hoja hizo, wakili Mwenda amedai ombi hilo atalifikisha kwa viongozi wake na tarehe ijayo watakuja na majibu.

Hakimu Shaidi baada ya kusikiliza hoja za upande zote aliutaka upande wa mashtaka kuhakikisha upelelezi unakamilika kwa wakati.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Novemba 25, 2019 itakapotajwa tena.

Mshtakiwa amerudishwa rumande kutokana na shtaka linalomkabili kutokuwa na dhamana.

Mbali na Twaleb, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ambao bado hawajafikishwa mahakamani ni raia wa Afrika Kusini, Phila Tshabalala na raia wanne wa Msumbiji; Henrique Simbue, Daniel Berdardo, Issac Tomu na Zacarious Junior.

Katika kesi ya msingi washtakiwa wanadaiwa kutenda makosa hayo kati  ya Mei Mosi, 2018 na Oktoba 10, 2018 katika maeneo mbalimbali ya jijini Dar es Salaam na Johannesburg,  Afrika Kusini.

Wanadaiwa kwa makusudi alitoa msaada wa kutendeka vitendo vya jinai au uhalifu wa kupangwa kwa lengo la kujipatia faida.

Oktoba 11, 2018 katika maeneo ya Hoteli ya Colloseum  iliyopo wilayani Kinondoni, Twaleb na wenzake  walimteka nyara Mo kwa nia ya kumhifadhi kwa siri na kumuweka maeneo ambayo ni hatari.

Julai 10, 2018 katika maeneo ya Mbezi Beach wilaya ya  Kinondoni, Twaleb na wenzake  walitakatisha Sh8 bmilioni wakati akijua fedha hizo ni kosa la kushiriki genge la uhalifu na makosa ya kupanga.