Anayedaiwa kumuua mfanyakazi wa ndani afikishwa kortini, waandishi wazuiwa

Muktasari:

Mahakama ya Wilaya ya Arumeru mkoani Arusha nchini Tanzania, imeahirisha kesi namba 5,2020 ya mauaji inayomkabili Mkazi wa eneo la Mianzini Arusha, Mkami Shirima (30) anayedaiwa kumuua mfanyakazi wake wa ndani Salome Zakaria (18) kwa kumpiga.

Arusha. Mkazi wa eneo la Mianzini jijini Arusha nchini Tanzania, Mkami Shirima (30) amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Wilaya ya Arumeru jijini humo

kujibu tuhuma za mauaji ya Salome Zakaria (18).

Mkamia amepandishwa kizimbani leo Ijumaa Machi 13, 2020 na kusomewa mashtaka yanayomkabili mbele ya hakimu mkazi  mfawidhi wa mahakama hiyo, Amalia Mushi.

Hata hivyo, wananchi waliofika kusikiliza kesi hiyo hawakuruhusiwa kuingia mahakamani wakiwamo waandishi wa habari.

Akizungumza na waandishi mara baada ya kuahirishwa kesi hiyo namba 5, 2020 ya mauaji hadi Machi 26, 2020, Hakimu Mushi amesema kesi hiyo imetajwa tu kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka kusikiliza shauri hilo.

Hakimu Mushi amesema polisi wamewazuia watu mahakamani kwa kuhofia baadhi ya wananchi bado na hasira dhidi ya mtuhumiwa huyo.

"Polisi wamewazuia kwa kuhofia baadhi ya wananchi kuwa bado na hasira Kali dhidi ya mtuhumiwa hivyo wasingeweza kuwaruhusu,” amesema Hakimu Mushi

Mkamia ambaye anadaiwa ni mke wa Polisi mkoani Arusha anatuhumiwa kumuua kwa kipigo Salome akimtuhumu kuhusika na kupotea Sh50,000 katika nyumba yake Machi 6, 2020.

Salome ambaye alikuwa mfanyakazi wa ndani kabla ya kufikwa na mauti alifungiwa ndani kama adhabu.

Wakati wa kesi hiyo ikiendelea, ulinzi ulikuwa umeimarishwa na polisi ili kuzuia watu kuingia mahakama.