VIDEO: Anayepumua kwa msaada wa mashine inayotumia umeme aomba msaada Tanesco

Hamad Awadhi 

Muktasari:

Hamad Awadhi (28), anayeishi kwa kutegemea mashine ya kumsaidia kupumua  anatumia Sh50,000 kulipa gharama za umeme kwa wiki na Sh100,000 kwa ajili ya kununua dawa zinazomsaidia pia kupumua. Amesema anatumia dawa hizo kwa wiki moja.

 


Dar es Salaam. Hamad Awadhi (28), anayeishi kwa kutegemea mashine ya kumsaidia kupumua ameliomba Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kumsaidia aondokane na gharama ya kulipa bili ya nishati hiyo kila mwezi.

Amesema anatumia Sh50,000 kulipa gharama za umeme kwa wiki na Sh100,000 kwa ajili ya kununua dawa zinazomsaidia kupumua. Amesema dawa hizo ndani ya wiki moja zinakuwa zimekwisha, kulazimika kununua nyingine.

Awadhi ameomba msaada huo leo Jumanne Septemba 3, 2019 nyumbani kwake Mogo, Kipawa jijini Dar es Salaam katika mahojiano na Mwananchi.

Amesema mbali na mashine hiyo na dawa, ikiwa umeme utakatika  hutumia Sh45,000 kwa ajili ya kununua mtungi wa oksijeni.

Amesema akitumia mtungi huo pekee baada ya saa 48 oksijeni inakuwa imekwisha.

“Ninawaomba Tanesco wanisaidie kupata huduma ya umeme kwa urahisi, sina kazi na mke wangu vilevile aliacha ili aniuguze.  Nimepambana sana nimegonga mwamba.”

“Ninaiomba Serikali katika hili nimekuwa tegemezi kwa malipo ya umeme na ipo siku huenda nikashindwa kuipata huduma hii,” amesema Awadhi.

Kaimu meneja wa Mawasiliano Tanesco, Leila Mhaji amesema wamepokea maombi ya Awadhi na wanayafanyia kazi, “Suala hili tumelipokea na linahitaji mchakato wa ndani, hivyo likikamilika tutaeleza tutamsaidiaje.”

“Wapangaji wenzangu wamekaa sana vikao kuhusu suala la umeme ninaoutumia, nashukuru mwenye nyumba ni mwelewa na mstaarabu na wapangaji wenzangu pia walishauri ninunue kipimo changu kinachoonyesha umeme ninaotumia ili iwe rahisi katika malipo.”

“Kwa kawaida kwa siku ninatumia umeme wa Sh8000, nikiweka umeme wa Sh15,000 huwa ni siku moja au mbili umeisha na ninatumia wa jumuiya, unapoiisha inabidi ninunue wakati mwingine sina hela,” amesema Awadh.

Julai 10 mwaka huu, Hospitali ya Taaluma na Tiba – Mloganzila ilimpa msaada wa mashine hiyo ya kumsaidia kupumua yenye thamani ya Sh4 milioni.

Awadhi alifikishwa Hospitali ya Taifa Muhimbili- Mloganzila Julai 9, 2018 na kuruhusiwa Julai 9, 2019 baada ya afya yake kuimarika.

 

Kujua undani wa habari hii soma gazeti la Mwananchi la kesho Jumatano Septemba 4, 2019