Anayetuhumiwa kufanya ramli chonganishi mikononi wa polisi

Muktasari:

Itawa Ming'hwa(47) mkazi wa kijiji cha Ibingo Wilaya ya Shinyanga anayetuhumiwa kufanya ramli chonganishi na kusababisha mauaji, hasa ya wanawake anashikiliwa na Jeshi la Polisi.

Shinyanga. Itawa Ming'hwa(47) mkazi wa kijiji cha Ibingo Wilaya ya Shinyanga anayetuhumiwa kufanya ramli chonganishi na kusababisha mauaji, hasa ya wanawake anashikiliwa na Jeshi la Polisi.

Akizungumza na waandishi wa habari jana Jumanne Januari 28, 2020 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Debora Magiligimba amesema Ming’hwa ambaye ni mganga wa kienyeji alijisalimisha polisi Januari 24, 2020.

Amesema wanamshikilia kwa ajili ya mahojiano akituhumiwa kufanya ramli.

Hivi karibuni Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Simon Sirro alipokuwa mkoani Shinyanga alimtaka mganga huyo kujisalimisha polisi, kuagiza polisi kumtafuta.

“Ni kweli tumemkamata Itawa kwa mahojiano kuhusu tuhuma za kupiga ramli chonganishi na kusababisha mauaji .”

“Mauaji yalitokea Shinyanga. Tunawaomba wananchi kuendelea kutupa ushirikiano kwa kutoa taarifa za siri ili kuwakamata wanaojihusisha na mauaji,” amesema kamanda huyo.

Diwani wa viti maalum, Shela Mshandete amesema matukio ya mauaji yanawafanya wananchi kuishi kwa hofu.