Asasi za kiraia Tanzania zabainisha upungufu wa kanuni za uchaguzi serikali za mitaa

Sunday September 15 2019

By Sharon Sauwa, Mwananchi [email protected] co.tz

Dodoma. Policy Forum Tanzania na Mtandao Waangalizi wa Uchaguzi Tanzania(Tacceo) wamebaini upungufu kwenye kanuni za uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika Novemba 24, 2019 ikiwemo fomu za matokeo kutokuwa na nafasi ya kutaja jina la kituo cha kupigia kura.

Akisoma tamko la asasi hizo leo Jumapili Septemba 16, 2019 jijini Dodoma, Mwenyekiti wa Policy Forum, Martina Kabisama amesema fomu za uteuzi hazibainishi wala kutambua wenye ulemavu walioonyesha nia za kugombea nafasi za uongozi.

“Fomu za mpiga kura hazina picha ya mgombea, hali inaweza kuleta ugumu wa utambuzi wa mpiga kura kuchagua mgombea anayemtaka hasa kwa mpiga kura asiyejua kusoma na kuandika,” amesema.

Hata hivyo, amesema maoni yao waliyoyatoa wakati wa utungaji wa kanuni yalichukuliwa kwa asilimia 70.

“Masuala mengi katika kanuni yamezingatiwa na kufanyiwa maboresho kama tulivyopendekeza. Policy Forum, Tacceo na wadau wengine tunaipongeza Serikali kwa kuzingatia takribani asilimia 70 ya maoni na mapendekezo yetu kama tulivyowasilisha,” amesema.

Martina amesema katika kanuni hizo kuna mkanganyiko wa majina ya kanuni kwa kuonyesha jina ni Kanuni za Uchaguzi kwa Mwenyekiti wa Kijiji, Wajumbe wa Halamashauri ya Kijiji na Mwenyekiti wa Kitongoji katika mamlaka za miji.

Advertisement

Hata hivyo, amesema katika mamlaka za miji hakuna kitongoji na badala yake ingesomeka kanuni za uchaguzi wa mwenyekiti wa kitongoji katika mamlaka za miji midogo.

Mwenyekiti huyo amesema kifungu kinachompa kinga msimamizi wa uchaguzi kinaweza kutumiwa vibaya kwa kisingizio cha nia njema kwa sababu kinazuia vyombo vya kutolea haki kutimiza wajibu wake na raia yoyote kukosa haki ya kudai katika vyombo hivyo.

Hata hivyo, Naibu Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, (Tamisemi) Josephat Kandege amesema haiwezekani kuzingatia mapendekezo ya kila mtu.

Advertisement