Ashikiliwa kwa kujiandikisha mara mbili katika daftari la wapigakura Morogoro

Muktasari:

  • Polisi mkoani Morogoro nchini Tanzania limetoa onyo kwa wananchi wa mkoa huo watakaothubutu kujiandikisha zaidi ya mara moja katika orodha la wapiga kura wa uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika Novemba 24, 2019 wanachukuliwa hatua.

Morogoro. Ngeze Mwagilo (29) mkazi wa Kasanga Manispaa ya Morogoro anashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kujiandikisha mara mbili katika daftari la wapigakura kwenye vituo viwili tofauti ndani ya manispaa ya Morogoro.

Kamanda wa polisi mkoani Morogoro, Wilibroad Mutafungwa amewaambia waandishi wa habari leo Jumanne Oktoba 15, 2019 ofisini kwake.

Amesema mtu huyo alikamatwa baada ya jeshi hilo kupata taarifa na kumfuatilia mtuhumiwa huyo wakati wa shughuli ya uandikishaji ikiendelea.

Mutafungwa amewatahadharisha wananchi mkoani humo wenye lengo la kutaka kuvuruga shughuli hiyo iliyoanza Oktoba 8 hadi 17, 2019 watachukuliwa hatua za kisheria kuwa polisi itahakikisha inawakamata huku akiwataka kuacha kufanya uhalifu huo.

Amesema mtuhumiwa huyo anadaiwa kujiandikisha katika kituo cha Kasanga kata ya Mindu na baadaye kwenda kujiandikisha katika kituo cha kiwanja cha Ndege kata ya Kiwanja cha Ndege Manispaa ya Morogoro.

Amesema mtuhumiwa huyo anaendelea kuhojiwa na atafikishwa mahakamani mara baada ya uchunguzi kukamilika ili sheria ichukue mkondo wake.

Hata hivyo, kamanda huyo amesema shughuli hiyo ya uandikishaji katika daftari la mpiga kura linaendelea kwa amani na utulivu kwani hakuna matukio yoyote yalioripotiwa ya uvunjifu wa amani mkoani Morogoro huku jeshi lake likiendelea na ulinzi katika maeneo mbalimbali.