Ashitakiwa kwa ugaidi baada ya kulamba vitu dukani kudhihaki corona

Muktasari:

Mtu mmoja nchini Marekani amefunguliwa mashitaka ya kutoa tishio la ugaidi baada ya kudaiwa kujirekodi akilamba vitu vilivyokuwa vinauzwa katika duka kubwa (supermarket) huku akisema “Nani anaogopa corona?”

Mtu mmoja nchini Marekani amefunguliwa mashitaka ya kutoa tishio la ugaidi baada ya kudaiwa kujirekodi akilamba vitu vilivyokuwa vinauzwa katika duka kubwa (supermarket) huku akisema “Nani anaogopa corona?”

Cody Pfister, mwenye umri wa miaka 26, alikamatwa baada ya video yake yenye kuudhihaki ugonjwa huo, ambao umeshaua maelfu ya watu duniani kote, kuamsha hasira sehemu mbalimbali duniani.

Picha za video zilizopigwa katika duka la Walmart jijini Warrenton katika jimbo la Missiouri zinamuonyesha mtuhumiwa huyo akivua barakoa na kulamba vitu kadhaa huku akiitazama kamera.

Maafisa jijini Warrenton walisema malalamiko kutoka kwa watu katika nchi mbalimbali, ikiwa ni pamoja na Uholanzi, Ireland na Uingereza, yaliwasaidia kumkamata mtuhumiwa huyo.

“Tunayapa malalamiko haya uzito mkubwa na tungependa kuwashukuru wale wote walioiripoti video hiyo ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa,” taarifa ya polisi ilisema.

Baada ya video hiyo kusambaa katika mitandao ya kijamii, mtangazaji Piers Morgan alitoa wito mtuhumiwa huyo akamatwe mara moja na kunyimwa tiba endapo angepata ugonjwa wa corona.