Asilimia 60 ya Watanzania kufikiwa na huduma ya bima mwaka 2024

Ofisa Mkuu wa wateja Binafsi, Biashara ndogo na za kati, Filbert Mponzi (kushoto) na Kamishna wa Bima kutoka katika Mamlaka ya Bima nchini (TIRA), Dk Mussa Juma wakizindua NMB Bancassurance. Katikati ni Meneja wa usimaimizi wa Fedha B.o.T, Mussa Sadat.

Muktasari:

Serikali kupitia Mamlaka ya Bima Tanzania (Tira) imejiwekea lengo ifikapo mwaka 2024 asilimia 60 ya Watanzania wawe wanapata huduma za bima na wanaelewa umuhimu wa bima.

Dar es Salaam. Serikali kupitia Mamlaka ya Bima Tanzania (Tira) imejiwekea lengo ifikapo mwaka 2024 asilimia 60 ya Watanzania wawe wanapata huduma za bima na wanaelewa umuhimu wa bima.

Kamishna wa Tira Mussa Juma ameyasema hayo wakati wa uzinduzi wa huduma ya bima kupitia benki inayotolewa na benki ya NMB.

Amesema ili kufikia azma hiyo, kampuni za bima, madalali wa bima, mawakala wa bima na benki zinazotoa huduma za bima zitalazimika kuongeza kasi ya kutoa elimu kwa Watanzania ili wapate kuelewa umuhimu wa kuziwekea bima mali zao.

Amesema wadau wa bima watalazimika kutumia teknolojia mpya ili kuwafikia watu wengi zaidi, wakiwemo wafanyabiashara wadogo,  baba na mama lishe.

Akizungumza katika uzinduzi huo, meneja mwandamizi wa Bima wa Benki ya NMB, Martin Massawe amesema uwepo wa matawi ya benki yake katika wilaya zote nchini kutasaidia kukuza sekta ndogo ya bima na kuinua mchango wake katika pato la taifa.

“Tulipata leseni ya kutoa huduma za bima mara baada ya kupitishwa kwa kanuni mwaka jana. Kutokana na kupatikana kwa matawi yetu katika wilaya zote nchini, tunaamini kupatikana kwa huduma za bima katika matawi yetu kutasaidia kukuza sekta ndogo ya bima,” amesema.

Ofisa mkuu wa wateja binafsi, biashara ndogo na za kati wa benki hiyo,  Filbert Mponzi amesema wameshatoa  bima kwa wafanyakazi wake wapatao 200 ambao wamethibitishwa kumudu utoaji wa huduma za bima kwa wateja.

“Tunaamini ujio wa NMB katika kutoa huduma za bima ni 'game changer' (ibadili mwenendo wa sekta) na kuipeleka sekta katika viwango vya juu,” alisema.

Amesema benki hiyo itatumia uwepo wa vilabu vya kibiashara katika maeneo mbalimbali nchini ili kueneza ujumbe wa umuhimu wa bima.

Huduma za bima zitakazopatikana katika matawi ya benki hiyo  ni za kampuni za Sanlam Life, UAP, Shirika la Bima la Taifa (National Insurance Corporation - NIC), Jubilee, Shirika la Bima la Zanzibar (Zanzibar Insurance Corporation – ZIC) na Reliance.