Asilimia 38 ya wasichana Tanzania hawajapata dozi saratani shingo ya kizazi

Muktasari:

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amesema kati ya wasichana 500,011 waliopata dozi ya kwanza ya chanjo ya saratani ya shingo ya kizazi mwaka 2018/2019,  asilimia 38 hawakurudi kwa ajili ya dozi ya pili ili kukamilisha chanjo kamili.

Dar es Salaam. Waziri wa Afya nchini Tanzania, Ummy Mwalimu amesema kati ya wasichana 500,011 waliopata dozi ya kwanza ya chanjo ya saratani ya shingo ya kizazi mwaka 2018/2019 asilimia 38 hawakurudi kwa ajili ya dozi ya pili ili kukamilisha chanjo.

Saratani ya shingo ya kizazi inaongoza kati ya saratani zote nchini kwa zaidi ya asilimia 36 huku ikiwa zaidi ya asilimia 40 kwa saratani zinazowakumba wanawake nchini.

Akizungumza leo Jumatatu Februari 3, 2020 wakati akizindua mwongozo wa matibabu ya saratani nchini, Ummy amesema  wasichana hao hawajamaliza chanzo kutokana na kutorudi kupata dozi ya pili.

Amesema chanjo hiyo ililenga kuwakinga wasichana wenye umri kati ya miaka 9 hadi 14, walengwa walikuwa wasichana wa miaka 14 kwa kuanzia ambao hata hivyo walezi na wazazi wameshindwa kuwafikisha vituo vya afya kwa ajili ya dozi ya pili.

“Katika kundi hili tuliweza kupata asilimia 81 pekee ya wasichana sawa na 500,011 walipata dozi ya kwanza, lakini ili chanjo ikamilike walitakiwa kupata dozi ya pili lakini kati yao asilimia 38 hawakurudi,” amesema.

Akizungumzia mwongozo huo, amesema tiba itakayotolewa na taasisi ya saratani ya  Ocean Road haitatofautiana na hospitali nyingine  binafsi na kwamba orodha ya dawa na vifaa tiba imeorodheshwa kwenye mwongozo huo.

Mkurugenzi wa Wizara ya Afya, Dk Grace Maghembe amesema mwongozo huo ulioanza kuandaliwa mwaka 2017, utahusisha hospitali za umma na binafsi kote nchini.