Asilimia 40 ya abiria wa ATCL wanatumia uwanja wa Mwanza

Muktasari:

Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) imeongeza uwezo wa kusafirisha abiria kutoka 4,000 mwaka 2016 hadi kufikia 62, 000 na mizigo kutoka tani tisa hadi tani 177 mwaka 2019.

Mwanza. Wapo waliokuwa wakihoji kwa nini Serikali ya Tanzania inafanya upanuzi wa uwanja wa ndege wa Mwanza kwa kiwango cha Kimataifa kwa nia ya kuweza kupokea ndege zote ndogo na kubwa.

Nadhani watu hao wamepata jibu leo Jumamosi Desemba 14, 2019 baada ya Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL), Ladislaus Matindi kusema uwanja huo ndiyo unasafirisha asilimia 40 ya abiria wote wanaosafiri kwa ndege za  ATCL.

Akitoa taarifa ya utendaji mbele ya Rais wa Tanzania, John Magufuli wakati wa hafla ya kupokea ndege mpya aina ya Bombardier Q-400 jijini Mwanza, Matindi kila siku, uwanja huo unahudumia abiria 1, 000 wanaosafirishwa kwa ndege za shirika hilo la umma.

“Idadi hii ni asilimia 40 ya abiria wote wanaosafiri kwa kutumia ndege za ATCL,” amesema Matindi

Kuhusu soko la usafirishaji kwa njia ya anga, Matindi amesema hadi sasa, ATCL inashikilia asilimia 75 ya umiliki wa safari za anga kutoka asilimia 73 za awali.

Kutokana kuimarika kiutendaji, Matindi amesema ATCL imeongeza uwezo wa kusafirisha abiria kutoka tani 4,000 mwaka 2016 hadi kufikia tani 62, 000 mwaka 2019.

Kwa upande wa mizigo, shirika hilo hivi sasa lina uwezo wa kusafirisha tani 177 ya mizigo kulinganisha na tani tisa za mwaka 2016.