Askofu Gamanywa aitaka CCM kumtunza Rais Magufuli

Muktasari:

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amekutana na viongozi wa dini mbalimbali kwa lengo la kuwaeleza miradi inayotekelezwa na Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais wa Tanzania, John Magufuli

Dar es Salaam. Kiongozi  wa Taasisi ya Wapo Mission International, Askofu Silvester Gamanywa amekiomba chama tawala nchini Tanzania cha CCM kumtunza Rais wa nchi hiyo, John Magufuli ili amalize kazi aliyoianza.

Askofu Gamanywa ameyasema hayo leo Jumatatu Novemba 18, 2019 wakati wa mkutano uliowakutanisha viongozi wa dini na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda uliokuwa na lengo la kuwaeleza viongozi hao wa kiroho miradi inayotekelezwa na Serikali ya awamu ya tano tangu iingie madarakani Novemba 5, 2015.

“Naomba CCM mtusaidie kumtunza Rais wetu, bado tunamtaka amalize kazi. Mtafanya mambo mengine baadaye mruhusuni amalize kazi.”

“Sizungumzii kuongezewa muda, namaanisha katika muda huohuo kazi aliyoianza apate kuimaliza. Simpigii debe mimi sio mwanasiasa najivunia nchi yangu,” amesema Askofu Gamanywa

“Huko nyuma nilikuwa naona haya kujitambulisha, sasa hivi naona fahari kujitambulisha kutokana na kazi nzuri iliyofanywa na nchi yetu,” amesema

Kuhusu kazi iliyofanyika katika uongozi wa Rais Magufuli, Askofu Gamanywa amesema kilichofanyika ni miujiza ya kisayansi na mikakati iliyopangwa na kutekelezwa na binadamu kwa nguvu.

“Tutakuwa hatujamtendea haki Mungu tusipowaambia waumini wetu kushukuru kwa kazi hii. Ninaamini kwamba haya yamewezekana kwa sababu Rais ana mcha Mungu na anamkiri hadharani na kiongozi yeyote anayemkiri hadharani Mungu anamjalia uweza.”

“Hii ndiyo rekodi katika historia ya Tanzania kwamba tunaitwa viongozi wa dini kupewa taarifa ya kazi alizofanya Rais. Tumezoea kuitwa kupewa ahadi lakini sio kupewa ripoti ya kilichoahidiwa kwenye kampeni,” amesema

Kiongozi huyo wa kiroho ametoa wito kwa viongozi wa dini kuwafundisha vijana kutii mamlaka ili kuwapunguzia kazi polisi na kuwaondolea ulazima wa kutumia nguvu.

“Tuwafundishe vijana wetu kutii mamlaka, tusiwape kazi polisi ambayo inaweza kuepukika. Tuwafundishe kuwa na adabu ili wote tufaidi matunda ya kazi nzuri,” amesema