Askofu Maboya amesema watafunga kwa siku saba kuwaombea wafiwa kufuatia vifo vya watu 20

Muktasari:

Askofu mkuu wa Kanisa la Calvary Assembles of God, Dustan Maboya amesema kanisa hilo litaendelea kufanya mikutano ya injili na kufunga siku saba kuwaombea ndugu wa wafiwa na kuwapa faraja kufuatia vifo vya watu 20 waliofariki katika kongamano lililofanyika Februari Mosi, 2020 mjini Moshi Mkoa wa Kilimanjaro.

Moshi. Askofu mkuu wa Kanisa la Calvary Assembles of God, Dustan Maboya amesema kanisa hilo litaendelea kufanya mikutano ya injili na kufunga siku saba kuwaombea ndugu wa wafiwa na kuwapa faraja kufuatia vifo vya watu 20 waliofariki katika kongamano lililofanyika Februari Mosi, 2020 mjini Moshi Mkoa wa Kilimanjaro.

Walifariki wakati wakigombea kukanyaga mafuta ya upako yaliyotolewa na Mtume na Nabii, Boniface Mwamposa. Katika kongamano hilo watu 16 walijeruhiwa.

Maboya amesema ataendelea kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi na kuwataka waumini wa kanisa hilo kukaa kimya, kutosikiliza yanayoendelea kwenye mitandao.

Amesema kwa sasa Mwamposa amepumzika kutokana na tukio hilo kwa kuwa limemfanya asiwe katika hali nzuri.

''Hili ni jambo zito sana kwetu na kwa Taifa kupoteza watu 20 kwa wakati mmoja sio jambo jepesi  ninawaomba waumini kuendelea kunyamaza,  msisikilize yanayoendelea kwenye mitandao. Tuliachie Jeshi la Polisi kuendelea kufanya kazi yake. Tutaendelea kuwapa ushirikiano,” amesema Askofu Maboya.