Askofu Malasusa asema Balozi Kaduma alijitoa kwa kanisa, tutamuenzi milele

Muktasari:

Kanisa la KKKT Dayosisi ya Mashariki na Pwani limesema Balozi Kaduma ameacha alama alipoamua kutoa kiwanja kwa ajili ya ujenzi wa kanisa hilo usharika wa Makongo Juu, Dar es Salaam.

Dar es Salaam. Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kirutheli Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Dk Alex Malasusa amesema watamuenzi mwanasiasa wa zamani nchini humo, Balozi Ibrahim Kaduma kutokana na mchango wake kwa kanisa hilo.

Amesema Balozi Kaduma ndiye aliyetoa kiwanja cha ujenzi wa kanisa hilo, Makongo Juu Dar es Salaam na kusimamia kamati ya ujenzi ya kanisa hilo.

Akizungumza katika ibada ya kuaga mwili wa kiongozi huyo leo Jumanne Septemba 3, 2019, Askofu Malasusa amesema kanisa hilo linamsifu Mungu kwa maisha ya kiongozi huyo ambaye alimthamini kila mmoja bila kujali ubaguzi.

Askofu Malasusa amesema ni heri kuondoka duniani vizuri kama mzee huyo kuliko kuharibu maisha na heshima iliyojengeka kwa muda mrefu wakati wa uzee.

"Mzee Kaduma alikuwa msema kweli, hakutaka kuzunguka na alitupatia kiwanja kwa bei ya shilingi sifuri hili kwetu linatupatia faraja kubwa sana," amesema Askofu Malasusa.

Ameitaja nafasi nyingine ya Balozi Kaduma kwenye kanisa hilo kuwa ni Mwenyekiti wa Fedha wa Chuo Kikuu cha Tumaini- Makumira na ameimba kwaya mbalimbali katika kanisa hilo.

Mtoto wake Yohane Kaduma amesema baba yake aliamini cheo, mamlaka, maslahi, shida na magonjwa kati yake hakuna kinachoweza kumtenganisha na upendo wa Mungu.

"Baba yetu alipenda watu wote bila ubaguzi akisisitiza kazi kwa bidii," amesema.

Yohane amesema baba yake alianza kuugua Julai 31, 2019 akiwa mkoani Arusha kwa binti yake baada ya matibabu alishauriwa kwenda kutibiwa zaidi katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Dar es Salaam.

Amesema baada ya matibabu, Muhimbili Agosti 29, 2019 alipelekwa nchini India na Agosti 31, 2019 alifariki dunia.

Awali, Askofu wa kanisa la AICT, Dayosisi ya Pwani, Charles Salala aliwataka Wakristo kutunza muda kwa kufanya mema kwa sababu ukipita haurejei.

Balozi Kaduma anasafirishwa kesho asubuhi Jumatano Septemba 4,2019 kwenda Kibena mkoani Njombe na atazikwa nyumbani kwake Alhamisi ya Septemba 5,2019.