Askofu Shoo, Dk Bashiru wamwombea msamaha Makonda, yeye ashangaa

Friday May 10 2019

 

By Waandishi Wetu,Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam/Hai. Ibada ya mazishi ya mfanyabiashara maarufu, Reginald Mengi jana iligubikwa na tukio la upatanisho, huku mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT), Askofu Fredrick Shoo na katibu mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally wakitaka viongozi vijana kuchunga ndimi zao.

Mengi, aliyefariki Mei 2 akiwa Dubai, Umoja wa Falme za Kiarabu, alizikwa jana kijijini kwao Nkuu, Machame na maisha yake yalitumika kama somo kwa viongozi wa kisiasa, walioungana na wananchi wengine kupumzisha mwili wa mwenyekiti huyo wa kampuni za IPP.

Askofu Shoo aliongoza ibada hiyo iliyofanyika Usharika wa Moshi Mjini mkoani Kilimanjaro, na alitumia mahubiri yake kuonya viongozi dhidi ya matumizi mabaya ya madaraka na kushauri kutumia utajiri kusaidia wengine, huku Dk Bashiru akitumia nafasi ya kutoa neno kueleza ya moyoni.

Wawili hao walikuwa wakirejea kilichosemwa awali na Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe. Katika hotuba yake fupi, Mbowe alizungumzia kauli aliyosema ina ubaguzi na kuomba radhi kwa niaba ya aliyeitoa.

Lakini, Dk Bashiru ndiye aliyemtaja mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kuwa alitoa kauli hiyo na akaungana na Mbowe kumuombea msamaha.

Wakati wa kuaga mwili wa Mengi siku nne zilizopita kwenye ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam, Makonda alimsifu Mengi kwa moyo wake wa kusaidia wasiojiweza, akisema tabia hiyo ni tofauti na Wachaga wengi.

Advertisement

“Sikuwahi kutegemea hata siku moja. Mchaga anatoa pesa kwa mlemavu? Ni jambo gumu sana. Mchaga anampa yatima pesa ni jambo ambalo haliwezi kuelezeka,” alisema.

“Mchaga anakubali kumpa mtu hata asiye na ndoto, matumaini? Si jambo rahisi na kwa hili nazidi kusema si tu kwamba tumepoteza Mchaga bora kati ya Wachaga wote, bali tumempoteza Mtanzania aliyekuwa zaidi ya kabila lake.”

Kauli hiyo ilisababisha watu wengi wamkosoe kwenye mitandao ya kijamii.

Jana, baada ya Dk Bashiru kumaliza kuzungumza, Askofu Shoo alimwita Makonda madhabahuni ili aombe msamaha huku akimueleza Wachaga, ambao wanatokea Mkoa wa Kilimanjaro, wamemsamehe.

Hata hivyo, Makonda alisita akionekana kutikisa kichwa huku waliokuwa karibu yake wakionekana kumuhimiza jambo.

Akiwa amevalia fulana, suruali aina ya jeans na koti, Makonda alikwenda madhabahuni kuteta jambo na Askofu Shoo, akionekana kama anayehoji sababu za kuomba radhi.

“Hapa madhabahuni ni sehemu ya upatanisho,” alisema Askofu Shoo.

Baada ya majadiliano kama dakika moja, Makonda alimwita Mbowe na akashikana naye mikono mbele ya Askofu Shoo kisha akapewa fursa ya kuzungumza.

“Mimi niombe radhi kwa tafsiri hiyo kwa sababu nimemsifia mchaga katikati ya wachanga siyo mchaga katikati ya kabila jingine,” alisema Makonda huku akifafanua kuwa alieleweka vibaya.

“Nitaendelea kumuenzi Mzee Mengi kwa mema yote aliyoyafanya kwa walemavu hasa katika mkoa wetu yatabaki kuwa alama.”

Mahubiri ya Askofu Shoo

Awali katika mahubiri yake, Askofu Shoo alisema kama kuna dhambi ambayo binadamu anapaswa kuifanyia toba, ni ya kubaguana na kama Watanzania wanahitaji taifa lipokee baraka kutoka kwa Mungu ni kuacha kufanya hivyo.

Alisema dhambi nyingine inayopaswa kufanyiwa toba ni ile ya watu wenye nafasi kuwakanyaga wengine.

Alisema jamii inapaswa kujifunza kwa kuangalia maisha Mengi kwa sababu alikuwa na nafasi ya kufanya mambo mengi, kama kununua haki za watu wengine.

“Kama kuna kitu tunaweza kumuenzi, ni kuiga roho yake ya upendo, kutokuwabagua watu kutokana na matabaka au kabila, “ alisema askofu huyo wa dayosisi ya Kaskazini.

“Nimemsikia mbunge wetu Freeman Mbowe akisema jambo fulani ambalo wakati mwingine huenda tunaongea kwa ndimi kuteleza. Tunaomba sana Mungu atusaidie.

“Tusibaguane kwa misingi yoyote ile, nimefuatilia malumbano yanayoendelea katika mitandao ya kijamii kati ya watu wa chama kimoja na chama kingine, nakuta maneno hadi najiuliza hivi ni Watanzania wameweza kufika mahali kwa namna hiyo?”

Askofu Shoo alisema Mengi alithamini maneno ya maridhiano kati ya Watanzania licha ya tofauti zao; matajiri, maskini wenye mamlaka, wasiokuwa na mamlaka na makabila.

Alisema hali imebadilika kwa kuwa hivi sasa kuna watu ambao wakipata fedha kidogo au cheo wanadharau wengine.

“Acha, acha kiburi. Namuomba Mungu atujaalie roho hiyo ya unyenyekevu,” alisema.

Pia aligusia suala la uhusiano wa Mengi na kanisa, akisema kuna watu wanaopenda kupotosha ukweli hata kama wanaufahamu.

Alisema baada ya kutokea msiba huo, watu walianza kuandika katika mitandao ya kijamii, wakihukumu maisha yake lakini akasema katika utaratibu wa kanisa mtu akitambua dhambi zake na kutubu, anarudishwa kundini na kwamba Mengi alifanya hivyo Oktoba 19, 2014.

“Mtu akisharudishwa kundini wewe mwanadamu mwenye dhambi kama mimi una nini zaidi la kusemea hapo. Acha,” alisema Dk Shoo.

Pia alitaka viongozi watetea haki na maslahi ya wananchi, akilitaka Bunge kufanya kazi yake ipasavyo.

“Huu ukawe ni ujumbe kwetu sote na Mungu atusaidie mkalishike hili, mkaendelee kuiombea familia na yale mazuri mengi tuliyojifunza kwake (Mengi) tukayatende,” alisema Dk Shoo.

“Nashukuru Mheshimiwa (Spika wa Bunge, Job) Ndugai uko hapa. Kazi ya Bunge ni kutetea maslahi ya wananchi. Teteeni maslahi ya wananchi mnaowawakilisha, kama kweli tunasema tumejifunza kutoka kwa Dk Mengi.”

Ni mara ya pili sasa

Akitoa salamu zake, Dk Bashiru alisema matunda ya kutoandaa viongozi bora yameanza kuonekana kwa vijana, akirejea suala la Makonda.

“Naomba nitumie fursa hii kumuombea msamaha kijana wangu Makonda. Mimi namfahamu na hii ni mara yangu ya pili namsema hadharani,” alisema Bashiru.

“Mara yangu ya kwanza nilimsema Simiyu akaja analia ofisini, nikasema ubadilike na kwa kweli ameanza kubadilika. Bado ni kijana mzuri, shupavu lakini tunahitaji kuwasaidia vijana wetu.”

Mbowe asema tumemsamehe

Awali Mbowe alikemea kauli za ubaguzi wa dini, rangi, ukabila na kisiasa.

“Kipekee kabisa mnisamehe. Niseme jambo moja ambalo limetukwaza wengi na kwa sababu sina tabia ya unafiki nitasema straight,” alisema Mbowe.

Mbunge huyo wa Hai alisema inapotokea kiongozi mwenye mamlaka akatoa kauli ya kubeza kabila fulani, watu wanaanza kubaguana kwa makabila au kwa dini.

“Tusianze kubaguana kwa itikadi, tusibaguane kwa imani, tusibaguane kwa makabila yetu, tupendane na kutambuana kama Watanzania, kauli za kuambiana kuwa kuna kabila fulani haliwezi kuwatetea walemavu si za kweli ni za kibaguzi na lazima tuzikemee,” alisema.

“Naomba wote walioguswa na kauli zile tutoe msamaha kumuenzi mzee wetu Mengi, tusamehe. Lakini tusiwe wanafiki tujifunze kusema ukweli na kweli itawaweka huru.”

Alisema katika mazingira ya kibinadamu kuna mambo mawili yanayojenga kiburi ambayo ni mamlaka yasiyotumiwa vizuri na fedha zisizotumika kwa unyenyekevu.

“Mzee Mengi hakuwa kiongozi wa kisiasa, lakini alikuwa mnyenyekevu. Utajiri wake haukumtia kiburi, bali ulimuongezea unyenyekevu na msaada kwa wengi ambao aliwajua na ambao hakuwajua,” alisema.

“Hivyo kuna kila sababu ya kumshukuru Mungu kwa maisha yake hapa duniani. Niombe sana Watanzania wenzangu kama tulivyokuwa kwa pamoja na kukaa pamoja kwa dini zote, kabila zote, vyama vyote niombe basi tuuendeleze unyenyekevu kwa siku zote na siyo tuuonyeshe tunapokuwa kwenye matatizo.”

Spika Ndugai

Naye Spika Ndugai alisema watu wanapaswa kujua ugumu wa kuwa spika na wajifunze kuchuja baadhi ya maneno yanayowekwa katika mitandao ya kijamii kwa sababu mengi si ya kweli na kwamba kazi ya uspika ni ngumu.

“Nafikiri baba askofu umeona ugumu wa kuwa spika. Umejaribu tu kidogo umeona wewe mwenyewe shughuli iliyotokea, kwa hiyo mnaposema kwenye mitandao ya kijamii kuhusu Job Ndugai mjue kazi ngumu niliyonayo,” alisema Ndugai.

Alisema vivyo hivyo kufanywa kwao huku akiwataka watu kutoamini kila kitu kinachoandikwa mle.

Advertisement