Askofu Shoo ahimiza mshikamano KKKT, ashukuru kwa kuaminiwa

Muktasari:

Saa chache baada ya kuchaguliwa tena kuwa mkuu wa kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk Frederick Shoo ameshukuru kwa kuaminiwa na kusisitiza waumini wa kanisa hilo kuendelea kuwa na mshikamano


Arusha. Saa chache baada ya kuchaguliwa tena kuwa mkuu wa kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk Frederick Shoo ameshukuru kwa kuaminiwa na kusisitiza waumini wa kanisa hilo kuendelea kuwa na mshikamano.

Katika uchaguzi uliofanyika usiku wa kuamkia leo Jumamosi Agosti 24, 2019 mjini Arusha, Dk Shoo alishinda kwa kupata kura 144 dhidi ya 74 za Askofu Abednego Keshamshahara wa Dayosisi ya Kaskazini Magharibi.

Kwa ushindi huo,  Dk Shoo anaendelea kuliongoza kanisa hilo kwa miaka mingine minne na kufuata nyayo za wakuu wa kanisa hilo waliomtangulia walioliongoza kwa vipindi viwili vya miaka minne. Alipata kura 144 kati ya  218.

Dk Shoo  amewashukuru waumini kwa kumuamini tena, kwamba kazi kubwa iliyopo mbele yao ni kuongeza umoja wa kufanya kazi kwa kumtegemea Mungu kama maandiko yanavyosema.

"Nawashukuru  wajumbe wa mkutano mkuu, nashukuru Askofu Keshamshahara na wengine wote kwa kuniamini na kunichagua,” amesema Dk Shoo.

Katibu Mkuu wa KKKT, Brighton Kilewa  alitangaza majina ya Dk Shoo na Keshamshahara yaliyopitishwa na kikao cha maaskofu huku uchaguzi huo uliokuwa na kila aina ya upinzani ukianza saa 10 jioni hadi saa 5 usiku.