MIAKA 20 BILA YA NYERERE: Azimio la Arusha lazaliwa, Kambona akimbia nchi-9

Muktasari:

Matokeo ya mkutano wa Halmashauri Kuu ya Tanu uliokutana mjini Arusha Januari 26 hadi 29, 1967 ni kile kilichojulikana baadaye kama Azimio la Arusha. Ingawa uamuzi huo ulipitishwa katika mkutano huo wa Arusha, Mwalimu Nyerere alilitangaza azimio hilo Februari 5, 1967 jijini Dar es Salaam katika Ukumbi wa Arnatoglu, Mnazi Mmoja na kuthibitishwa na Mkutano Mkuu wa Tanu Machi 1967. Mwandishi William Shao anafafanua zaidi kuhusu tukio hilo la kihistoria...

Inawezekana mlolongo wa mambo yote haya yaliyotufikisha kwenye Azimio la Arusha ulianzia Februari 1966 Serikali ilipochapisha muswada wa sheria wenye madhumuni ya kuanzisha programu ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), mpango ambao baada ya hapo ulisimamiwa na wakufunzi wa kijeshi kutoka Israel.

Mawazo ya kuanzishwa JKT yalitokana na Umoja wa Vijana wa Tanu (TYL) katika mkutano wao mkuu uliofanyika Agosti 25, 1962 mjini Tabora chini ya Katibu Mkuu wao, Joseph Nyerere. Aprili 19, 1963 Baraza la Mawaziri likapitisha azimio hilo na likaanzishwa Jumatano ya Julai 10, 1963.

Kufikia mwaka 1966, ilionekana kuna umuhimu wa vijana wasomi wenye elimu zaidi ya kidato cha nne kulitumikia JKT. Kwa sababu hiyo moja sheria ilirekebishwa ili kuipa JKT nguvu za kisheria kuandikisha vijana wenye taaluma zaidi ya kidato cha nne kwa mujibu wa sheria.

Mpango huo sasa ukawa ni lazima kwa wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kilichoanzishwa mwaka 1961 na ambacho sasa kilikuwa kinatoa wahitimu wa kwanza ambao, kwa namna fulani, walionekana tishio kwa vyeo vya baadhi ya viongozi serikalini.

Wanafunzi hao walitakiwa kwenda kambini kwa miaka miwili. Miezi sita ya mwanzo ikiwa ni ya mafunzo ya kijeshi na mingine 18 ni ya kutumikia jeshi nje ya kambi kama watumishi wa umma. Walitakiwa pia kukatwa asilimia 60 ya mishahara yao kama mchango wa kulitumikia taifa.

Wanafunzi hao waligoma na kisha kuandamana. Mojawapo ya mabango waliyokuwa nayo liliandikwa ‘Afadhali wakati wa Ukoloni.’ Viongozi wao walikuwa ni Samuel Sitta na Wilfred Mwabulambo (wote sasa ni marehemu). Hata hivyo kiasi cha wanafunzi 400 walifukuzwa na chuo kikafungwa kwa miezi tisa hadi waliporudishwa chuoni.

Huu ulikuwa ni mwanzo wa kubadili sera, siasa, mtazamo na mwelekeo wa Serikali ya Mwalimu Nyerere. Siku chache baada ya kukifunga chuo hicho, Mwalimu alianza ziara mikoani akiwahutubia wananchi wa vijijini na mijini kuhusu hali halisi ya nchi na mipango mipya ya kuendesha nchi.

Hatimaye ziara zake ziliishia mjini Arusha. Katika hotuba yake ya Jumatatu ya Januari 23, 1967 kwa wakuu wa mikoa ndipo alipoanza kuweka hadharani mawazo yake kuhusu siasa aliyoitaka, na ndipo alipoitisha mkutano wa Halmashauri Kuu ya Tanu ujadili suala hilo, ambalo matokeo yake ni Azimio la Arusha.

Akifungua kikao cha mkutano huo Alhamisi ya Januari 26, Mwalimu Nyerere alitumia zaidi ya saa tatu akielezea Ujamaa na faida zake.

Azimio lilisema kuwa kiongozi wa Tanu au wa Serikali ni sharti awe mkulima au mfanyakazi, na asishiriki jambo lolote la Kibepari au Kikabaila, asiwe na hisa katika makampuni yoyote, asiwe mkurugenzi katika kampuni ya kikabaila au kibepari, asiwe na mishahara miwili au zaidi na asiwe na nyumba ya kupangisha.

Oscar Salathiel Kambona ambaye alikuwa mwandani na msiri mkubwa wa Mwalimu Nyerere tangu wakati wa ujenzi wa chama cha Tanu mwishoni mwa miaka ya 1950, alianza kupingana naye juu ya sera zake. Wakati Nyerere akielekea zaidi kwenye Ujamaa, Kambona alikuwa akielekea kwenye Ubepari.

Mkutano huo wa Arusha uligeuka kuwa ubishani mkali wa hoja. Katika mkutano huo Nyerere alipendekeza Ujamaa uwe ndiyo sera kuu ya serikali ya Tanzania, lakini Oscar Kambona alipinga vikali sera hiyo. Katika ukurasa wa 172 wa kitabu chake, ‘The African Liberation Struggle: Reflections’, mwandishi Godfrey Mwakikagile ameandika kuwa mara kwa mara mkutano ulilazimika kuvunjika ili kuwaruhusu viongozi wao watatu Nyerere, Kambona na Kawawa kwenda kufanya mazungumzo faraghani, waelewane ndipo warudi kikaoni kuendelea na mkutano.

“Lakini kila waliporejea kwenye mkutano ilionekana dhahiri kwamba Kawawa alikuwa upande wa Nyerere dhidi ya Kambona,” anaandika Mwakikagile.

Kila jambo lililoleta mtafaruku mkubwa kwenye kikao hicho ilibidi pawepo na vikao vya siri ili kuweka mambo sawa kabla ya kurejea katika hadhara kuendelea na mkutano, na mjadala mwingine mkubwa uliotawala siku iliyofuata ulikuwa ni ama Tanzania iwe na vijiji vya ujamaa katika mpango wa kufuata mfumo wa ujamaa au vinginevyo, na katika mijadala hiyo Rashid Kawawa alikuwa anakubaliana na kila alilosema Mwalimu Nyerere kumpinga Kambona na baadhi ya wachache wengine.

Kambona alikuwa kiongozi pekee wakati huo aliyeweza kutoa ushauri na kumpinga Nyerere pale alipoona nafsi yake haijaridhika na mpango ulioamriwa na alimwona Nyerere kama binadamu mwingine au sawa sawa naye.

Pamoja na mambo mengine, msingi mkubwa wa tofauti baina ya Kambona na Nyerere katika kuanzishwa kwa Azimio la Arusha ilikuwa ni Vijiji vya Ujamaa. Kambona hakupenda kabisa mfumo wa ujamaa kama alivyotaka Mwalimu Nyerere.

Pamoja na upinzani mkali aliokuwa nao Kambona dhidi ya wazo la ujamaa la Mwalimu Nyerere, hatimaye Azimio la Arusha lilipitishwa katika kikao cha mwisho cha mkutano wa Arusha kilichomalizika Jumapili ya Januari 29 na hatimaye kutangazwa rasmi Jumapili ya Februari 5, 1967.

Sasa Tanzania ikajulikana rasmi kuwa ni nchi inayofuata uchumi wa ujamaa na Kambona akashindwa.

Azimio hilo liliona kwamba namna ya pekee ya kujenga na kudumisha ujamaa ni kuthibitisha kuwa njia kuu zote za uchumi wa nchi zinatawaliwa na kumilikiwa na wakulima na wafanyakazi wenyewe kwa kutumia vyombo vya serikali yao na vyama vyao vya Ushirika. Pia ni lazima kuthibitisha kuwa chama kinachotawala ni chama cha wakulima na wafanyakazi.

Njia kuu za uchumi zilizotajwa ni kama vile ardhi, misitu, madini, maji, mafuta na nguvu za umeme; njia za habari, njia za usafirishaji; mabenki, na bima; biashara; biashara na nchi za kigeni na biashara za jumla; viwanda vya chuma, mitambo, silaha, magari, simenti, mbolea, nguo, na kiwanda chochote kikubwa ambacho kinategemewa na sehemu kubwa ya watu katika kupata riziki zao au kinachotegemewa na viwanda vingine; mashamba makubwa na hasa yale yanayotoa mazao ya lazima katika viwanda vikubwa.

Ingawa aliendelea kuwa waziri katika Serikali ya Nyerere, aliondolewa katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ulinzi na kupewa Wizara ya Serikali za Mitaa na Maendeleo Vijijini.

Nyerere alipogundua kuwa Kambona alitembelea Ujerumani Mashariki na Urusi bila taarifa rasmi, wasiwasi wake juu ya Kambona uliongezeka. Uvumi uliposambaa jijini Dar es Salaam ukidai kwamba Kambona alikuwa anakula njama za kumpindua Rais wake, Nyerere alianza uchunguzi wa kimya kimya.

Kambona alipogundua kuwa anachunguzwa na kufuatiliwa, Ijumaa ya Juni 9, 1967 alijiuzulu nafasi zake zote, uwaziri na ukatibu mkuu wa Tanu kisha akaondoka yeye yeye na familia yake wakavuka mpaka na kuingia Nairobi, Kenya ambako walipanda ndege kwenda uhamishoni nchini Uingereza. Nyerere akawa mshindi katika kuanzisha Azimio la Arusha. Kuanzia hapo yakafanyika matembezi karibu nchi nzima ya kuunga mkono Azimio la Arusha.

Mhanga wa kwanza wa Azimio la Arusha ni kijana mmoja aliyeitwa Seti Benjamin Mpinga (20), ambaye wakati akiwa kwenye matembezi ya kuunga mkono azimio hilo kutoka Arusha kuelekea Dar es Salaam kwa mguu, alipata matatizo ya kiafya akiwa njiani na kufariki dunia siku ile ile azimio hilo lilipotangazwa.

Seti alikuwa anawaongoza vijana 14 kutoka tawi la Umoja wa Vijana la Ussa River wakiongozwa kwenda Arusha mjini, mahali lilipozaliwa Azimio, na baadaye kuanza safari ya kwenda Dar es Salaam.

Hata hivyo, Azimio hili lilidumu kwa miaka 24 tu. Mwaka 1991 Halmashauri Kuu ya CCM ilikutana mjini Zanzibar na kufanyia mabadiliko azimio hilo na kuzaliwa kilichoitwa Azimio la Zanzibar. Mwenyekiti wa CCM, Ali Hassan Mwinyi, alikaririwa akisema “Hali yetu ya sasa hasa ya kiuchumi, si ile ya mwaka 1967.”

Itaendelea kesho