Balozi Mpungwe: Mufuruki alianza biashara na mtaji wa kompyuta moja

Muktasari:

  • Balozi wa zamani wa Tanzania nchini Afrika Kusini, Ami Mpungwe amesema mfanyabiashara maarufu nchini, Ali Mufuruki alianza biashara akiwa na mtaji wa kompyuta moja.

Dar es Salaam. Balozi wa zamani wa Tanzania nchini Afrika Kusini, Ami Mpungwe amesema mfanyabiashara maarufu nchini, Ali Mufuruki alianza biashara akiwa na mtaji wa kompyuta moja.

Ametoa kauli hiyo leo Jumanne Desemba 10, 2019 katika shughuli ya kuaga mwili wa Mufuruki katika ukumbi wa kimataifa  wa Julius Nyerere (JNICC).

Mwili wa Mufuruki aliyefariki dunia juzi alfajiri uliwasili nchini jana jioni ukitokea Afrika Kusini, baada ya kuagwa leo  utazikwa katika makaburi ya Kisutu, jijini Dar es Salaam.

Viongozi, wastaafu, wafanyabiashara na wananchi wamejitokeza katika ukumbi huo idadi ambayo inaibua tafsiri kuwa mfanyabiashara huyo alikuwa akigusa maisha ya wengi.

Katika maelezo yake,  Balozi Mpungwe aliyejuana na Mufuruki zaidi ya miaka 20 iliyopita amesema mfanyabiashara huyo aliacha kazi nchini Ujerumani na  kurejea Tanzania.

Amesema hekima, unyenyekevu, uwezo wa akili aliokuwa nao darasani ndio ulimwezesha kushiriki midahalo ya ndani na nje ya Tanzania lakini kuaminiwa na taasisi mbalimbali.

Akizungumzia Mufuruki alipoanzisha  kampuni ya Infotech Computer Limited mwaka 1989 amesema," alikuwa na mtaji wa kompyuta moja aliyotoka nayo chuo. Lakini  uwezo wake, ubunifu wake ndio ulikuwa mtaji mkubwa."

"Ali alikuwa mtu mwenye uwezo wa kipekee kufikiria masuala mbalimbali na uwezo wake darasani ulikuwa mkubwa sana uliomuwezesha kushiriki midahalo ndani na nje ya nchi.”

Huku mamia ya waombolezaji wakimsikiliza Balozi Mpungwe amesema, “alikuwa mtu wa kuaminika sana, wakati wote amekuwa mkweli, anapotoa mawazo yake anayasimamia na kuyatetea. Akikuahidi kitu atakifanya. Ali alikuwa muumini wa weledi kwa kufuata misingi iliyowekwa katika taasisi mbalimbali kama mjumbe wa bodi, mwenyekiti na hata ofisini kwake."

Balozi Mpungwe amesema Mufuruki alikuwa kiongozi wa familia yake, mke wake Saada Ibrahim na watoto wake, alikuwa kiongozi wa kukuza maadili.