Balozi wa Marekani ataka wasichana wawezeshwe

Kaimu Balozi wa Marekani Dk Inmi Patterson akiongea na mkutano wa ujasiriamali ulioandaliwa na Taasisi ya kuwawezesha wasichana Apps and Girls.

Muktasari:

Kaimu Balozi wa Marekani Dk Inmi Patterson amesema msichana anaweza kuleta mabadiliko katika jamii kama atawezeshwa na kupewa mafunzo bora ya kujitegemea

Dar es salaam. Msichana anaweza kuleta mabadiliko katika jamii kama atawezeshwa na kupewa mafunzo bora ya kujitegemea.

Hayo yameelezwa leo Ijumaa Desemba 13,2019 na Kaimu Balozi wa Marekani Dk Inmi Patterson wakati wa mkutano wa ujasiriamali ulioandaliwa na Taasisi ya kuwawezesha wasichana Apps and Girls.

Amesema wasichana wanapotunzwa vizuri wanakuwa katika nafasi nzuri, hivyo msichana na mvulana hawana tofauti kila mtu anatakiwa kuishi maisha huru ya kujitegemea.

“Ili mtu ufike pale unapotaka unahitaji elimu bora na mafunzo bora hivyo Ubalozi wa Marekani unaunga mkono mafunzo ya ujasiriamali yanayotolewa kwa wasichana ambayo yatawawezesha kuwa na utashi wa kujitegemea,”amesema Dk Patterson

Mwanzilishi wa Taasisi ya Apps and Girls, Carolyne Ekyarisiima, amesema wanatoa mafunzo ya Tehama kwa wasichana wa sekondari wanaosoma kwenye shule za serikali wa umri wa miaka 13 hadi 24.

Amesema mafunzo hayo yatawawezesha kuchagua masomo ya sayansi na kuwa na uwezo wa kutumia teknolojia na ujasiriamali kubuni vitu tofauti tofauti.

“Lengo la mafunzo haya ni kuweza kuwa na biashara au kampuni itakayowawezeha kuzalisha fedha zitakazowasaidia katika maisha yao,”amesema Ekyarisiima.

“Kama taasisi tumekuwa tukizunguka kwenye shule na kutoa mafunzo kwa wasichana namna ya kutumia kompyuta na baada ya hapo wanatakiwa kufikiria mradi ambao utatumia teknolojia,”amesema.

Ameongeza kuwa baada ya kutengeneza mradi au vifaa vinavyotumia teknolojia wanaongezewa ujuzi wa kibiashara utakaowawezesha kuwa na kampuni itakayobadilisha maisha yao.

Mkurugenzi wa Shirika la Msichana Initiative Rebecca Gyumi, amesema teknolojia inaweza kutatua changamoto na kuongeza fursa za ajira kwenye jamii.

Amesema kama wasichana watakataa tafsiri zinazodidimiza na kwenda mbele kwa kutafsiri kwa vitendo wanayo nafasi kubwa ya kufanya mabo makubwa.

“Wasichana wenyewe wanapaswa kuwa mstari wa mbele kubadilisha dhana ya kuonekana ni dhaifu kuonekana kazi fulani inatakiwa kufanywa na mwanamke na nyingine kufanywa na mwanaume” amesema Gyumi.

Amebainisha kuwa jamii inaweza kubadili mtazamo kwa kuweka malezi bora kwani Dunia imebadilika ili kuweza kufanya mambo makubwa mwanamke anapaswa kupewa nafasi.