Bandari ya Musoma Tanzania kufufuliwa

Meneja wa Bandari za Ziwa Victoria, Morris Mchindiuza

Muktasari:

“Tunakarabati Link Span (Daraja la kuungasha treni na meli), tunatarajia kutumia Sh650 milioni na ujenzi utakamilika Aprili, 2019, hii itasaidia kuboresha usafirishaji wa mazao ya kama pamba na kahawa sanjari na bidhaa za majini kutoka Musoma kwenda maeneo mengine.”

Mara. Mamlaka ya Bandari Musoma imesema ipo katika mpango wa kuifufua bandari ya Musoma ili kuboresha usafirishaji wa watu na bidhaa kutoka mkoani humo kuelekea maeneo mengine ya pembezoni mwa ziwa Victoria ndani na nje ya nchi.

Leo Ijumaa Desemba 6, 2019, Meneja wa Bandari za Ziwa Victoria, Morris Mchindiuza, amesema miaka 10 iliyopita bandari hiyo imekuwa haifanyi kazi lakini endapo itafufuliwa itakuwa na manufaa makubwa katika uchumi wa eneo hilo na Taifa kwa ujumla.

“Tunakarabati Link Span (Daraja la kuungasha treni na meli), tunatarajia kutumia Sh650 milioni na ujenzi utakamilika Aprili, 2019, hii itasaidia kuboresha usafirishaji wa mazao ya kama pamba na kahawa sanjari na bidhaa za majini kutoka Musoma kwenda maeneo mengine,” amesema.

Mchindiuza amesema Mamlaka ya Bandari inaendelea kutafuta masoko ya bandari hiyo na tayari kuna wafanyabiashara wameahidi kuitumia kusafirisha bidhaa zao kwa sababu ni usafiri wa maji ni nafuu ukilinganishwa na barabara inayotumika sasa.

Amesema bandari hiyo ambayo ilianza kutumika mwaka 1968 zamani ilikuwa ikihudumia meli zinazoiunganisha Musoma na Nchi za Uganda na Kenya sanjari na mikoa inayozunguka ziwa Victoria.

Aidha, mbali na Musoma Mamlaka ya bandari inakarabati madaraja kama hayo katika bandari ya Mwanza kusini na Kemondo Mkoani Kagera, Treni ikileta mzigo inasukuma mabehewa yake yenye mzigo kuingia kwenye meli kisha kusafirisha kueleka eneo jingine kwa ajili ya kushushwa.