VIDEO: Barabara zafungwa Moshi, wananchi wafurika kanisani ibada mazishi ya Mengi

Thursday May 9 2019

 

By Daniel Mjema, Mwananchi [email protected]

Moshi. Haijapata kutokea. Ndivyo unavyoweza kusema kutokana na umati wa watu waliojitokeza katika ibada ya mazishi ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Kampuni za IPP, Reginald Mengi.

Barabara zote za kuingia na kutoka katika Kanisa Kuu la Usharika wa Moshi mjini wa Dayosisi ya Kaskazini ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), zimefungwa kwa kuwekewa utepe wa njano na polisi.

Barabara ya kuelekea kanisa hilo ukitokea ofisi ya mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro imefungwa kuanzia jengo la NSSF Commercial Complex, wakati ile ya kutokea barabara ya Boma kuelekea kanisani imefungwa kuanzia ilipo benki ya KCB.

Halikadhalika barabara zinazoingia katika kanisa hilo kutokea eneo la kituo kikuu cha mabasi nazo zimefungwa, huku polisi wakiwamo wa kikosi cha usalama barabarani  wenye sare na wasio na sare wakiimarisha ulinzi kanisani hapo.

Hadi saa 3:30 asubuhi, kanisa lilikuwa limefurika waombolezaji ndani na nje kwenye mahema huku waombolezaji wengi wakifuatilia ibada hiyo nje ya uzio wa kanisa na eneo la mita za mraba 100 kuzunguka kanisa hilo.

"Sijawahi kuona umati mkubwa kiasi hiki katika kanisa letu. Hii inadhihirisha mzee Mengi aliishi kwenye mioyo ya Watanzania," alisema Davis Mosha aliyewahi kugombea Ubunge Jimbo la Moshi mwaka 2015.

Advertisement

Mbali na viongozi wa kisiasa, wasanii na wanamuziki nao wameshiriki ibada hiyo wakiwamo, Jackline Wolper, TID, Keisha.

 

Advertisement