Barrick kupunguza wafanyakazi North Mara

Dar es Salaam. Kwa mara ya tatu sasa ndani ya miaka minne, kampuni ya Barrick imetangaza kupunguza wafanyakazi katika Mgodi wa North Mara ili kumudu gharama za uendeshaji.

Mgodi huo uliokuwa unamilikiwa na Acacia hivi sasa upo chini ya kampuni ya Twiga iliyoundwa kwa ubia wa Serikali na Barrick Gold Corporation iliyokuwa kampuni mama ya Acacia.

Kwa mujibu ya taarifa iliyotumwa kwa wafanyakazi Januari 13, uamuzi huo unatokana na tathmini iliyofanywa kubaini kama mgodi huo una wafanyakazi wenye taaluma zinazohitajika wakitekeleza majukumu yanayowahusu ama la.

“Kwa kuzingatia sheria ya nchi tunawajulisha wafanyakazi wote, na nakala tukiwa tumeipeleka Numet (Chama cha Wafanyakazi Mgodi wa North Mara) kuhusu dhamira hiyo,” inasomeka sehemu ya taarifa hiyo iliyotolewa na meneja wa mgodi huo, Luiz Correia.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, upunguzaji huo utawahusu wafanyakazi 110 kutoka idara ya rasilimaliwatu, uchimbaji, usimamizi wa mali pamoja na ugavi.

Wengine watakaoathirika ni kutoka idara ya uhandisi mitambo, huduma kwa jamii, mazingira na usalama kazini.

Meneja wa mgodi huo, Correia alisema pazia la mawasiliano kati ya uongozi na chama cha wafanyakazi limefunguliwa wakati wafanyakazi wakisubiri matokeo ya uamuzi utakaoafikiwa na pande hizo mbili.

Numet kinasimamia masilahi ya waajiriwa mgodini hapo.

“Uongozi unatambua ugumu uliopo miongoni mwa wafanyakazi kuhusu kupunguzwa kazi lakini utachukua tahadhari zote muhimu kuhakikisha hakuna madhara yanayojitokeza na kulinda masilahi ya wafanyakazi, biashara na wadau wengine,” alisema meneja huyo.

Alisema mchakato huo utazingatia sheria zote za nchi kuhakikisha kila anayeguswa anapata stahiki zake hivyo akawataka wafanyakazi kuwa watulivu wakiendelea na majukumu yao.

Septemba 2018 Mgodi wa Bulyanhulu, miongoni mwa mitatu inayomilikiwa na Twiga kwa sasa ulitangaza kupunguza wafanyakazi kwa sababu za kiuendeshaji.

Mwaka mmoja kabla, Septemba 2017, kampuni hiyo ilipunguza wafanyakazi katika Mgodi wa Bulyanhulu kutokana na sababu za ukata pia uliochangiwa na kuzuiwa kwa usafirishaji wa makinikia nje ya nchi.

Mwaka 2017 Serikali ilizuia uuzaji wa makinikia nje ya nchi na kuwataka wachimbaji wa dhahabu nchini kujenga mitambo ya uchenjuaji ili kuongeza ajira kwa Watanzania.

Uamuzi huo uliofanywa na Rais John Magufuli ulitokana na ripoti za kamati mbili alizoziunda ili kufuatilia mwenendo wa biashara ya madini nchini.

Licha ya ripoti hizo, Bunge lilifanya mabadiliko ya sheria iliyopendekeza masuala kadhaa ikiwamo dhahabu kuanza kuhifadhiwa kama sehemu ya hazina ya Taifa.