Bashe apiga ‘stop’ uagizaji magunia nje ya nchi kuanzia mwaka 2020

Thursday December 12 2019

Naibu Waziri wa Kilimo nchini Tanzania, Hussein

Naibu Waziri wa Kilimo nchini Tanzania, Hussein Bashe 

By Mwandishi Wetu, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Naibu Waziri wa Kilimo nchini Tanzania, Hussein Bashe amesema kuanzia mwaka 2020 haitaruhusiwa magunia ya korosho kutoka nje kuingia nchini, badala yake yatatengenezwa na viwanda vya ndani.

Mbunge huyo wa Nzega Mjini ametoa kauli hiyo juzi katika

mkutano na wananchi wa halmashauri ya Wilaya ya Nzega mkoani Tabora akihamasisha zao la korosho wilayani humo.

Amesema kutokana na viwanda vya ndani kuwa na uwezo wa kutengeneza magunia yanayoweza kutosheleza mahitaji hakutakuwa na haja ya kuagiza kutoka nje.

“Mwaka huu  tumeagiza magunia kwa ajili ya korosho yenye thamani ya Sh16 bilioni,  kama nchi tuna katani na tuna watu walipewa viwanda kwa ajili ya kuzalisha magunia kwa hiyo mwaka kesho hakuna kuagiza magunia ya korosho, tutazalisha wenyewe ndani ya nchi,” amesema Bashe.

Amesema kuwa kuingiza magunia kutoka nje ya nchi ni gharama ikilinganishwa na yanayotengenezwa nchini.

Advertisement

“Ni aibu viwanda vyetu vya magunia tumevifunga halafu tunawapa watu tenda wanaenda kutuletea magunia kutoka India, Indonesia yanakuja nchini  maana yake tunaongeza gharama ya bili yetu ya importation (uingizaji) kwa hiyo tutaanza na zao la korosho, inawezekana,” amesema Bashe.

Amesema kama viwanda vya ndani vitazalisha kwa kiwango kinachotakiwa vina uwezo wa kukidhi mahitaji ya magunia kwa ajili ya kufungashia korosho.

“Mahitaji ya magunia ya korosho katika nchi ni kati ya gunia milioni 3 mpaka 4, viwanda vilivyopo vina uwezo wa kuzalisha zaidi ya magunia milioni 10 kwa mwaka,” amesema Bashe.

Amesema kuzalisha magunia yanayokidhi mahitaji ni suala la kufanya uamuzi ili kufungamanisha zao la korosho, katani na viwanda vilivyopo nchini.

Amewataka wenye viwanda vya kuzalisha magunia nchini kuweka wazi changamoto zinazowakabili kwenye uzalishaji ili Serikali iweze kuzifanyia kazi.

“Waliobinafsishiwa viwanda vya kuzalisha magunia kama wana changamoto wazilete serikalini tuzijadili kipindi hiki cha msimu wa kilimo, tutakapovuna korosho mwaka kesho ushirika hakuna kuagiza magunia kutoka nchi za nje.”

“Kama kuna matatizo kwa wazalishaji tukae nao, tujue tatizo lao ni nini ili tufungamanishe korosho, katani na viwanda,” amesema.

 

Advertisement