Bavicha, wazee kuchagua viongozi leo

Muktasari:

Wajumbe wa mkutano wa  Baraza la Vijana la chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania Chadema (Bavicha) na Baraza la Wazee leo Jumatatu Desemba 9, 2019 wanafanya uchaguzi wa viongozi wa baraza hilo.

Dar es Salaam. Wajumbe wa mkutano mkuu wa Baraza la Vijana la chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania Chadema (Bavicha), wameanza kuingia ukumbini wakisubiri kuanza kwa mkutano huo utakaokuwa na ajenda ya kuwachagua viongozi ngazi ya uenyekiti na makamu wake.

Mkutano huo unafanyika leo Jumatatu Desemba 9, 2019 katika ukumbi wa mikutano wa Mlimani City Dar es Salaam na tayari wajumbe wa Bavicha kutoka mikoa mbalimbali wameshawasili wakisubiri mchakato huo.

Kabla ya kuingia ndani, baadhi ya wajumbe hao walionekana katika makundi mbalimbali wakikaa na kuzungumza lile na hili kuhusu wagombea wa nafasi mbalimbali za Bavicha.

Katika uchaguzi huo utakaohudhuriwa na Katibu mkuu wa Chadema, Dk Vincent Mashinji utahusisha nafasi ya mwenyekiti atakayechukua nafasi ya Patrick Ole Sosopi ambaye atakuwa anamaliza muda wake sambamba na makamu uenyekiti wa Tanzania Bara na Visiwani.

Sosopi anamaliza uongozi wake akiwa mwenyekiti nafasi aliyoichukua kutoka kwa Patrobas Katambi ambaye Septemba 2014 ndiye alichaguliwa kuwa mwenyekiti huku Sosopi akichaguliwa kuwa makamu mwenyekiti- Bara wa baraza hilo.

Hata hivyo, Novemba 21, 2017 Katambi alijiunga na Chama cha Mapinduzi (CCM) na mwaka 2018, Rais wa Tanzania, John Magufuli alimteua Katambi kuwa Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini.

Baada ya Katambi kutimkia CCM, nafasi yake ilichukuliwa na Sosopi ambaye leo anakabidhi wadhifa hao kwa mwingine atakayechaguliwa.

Wanachuana katika nafasi ya uenyekiti ni John Pambalu, Dorcas Mwilafi na Mathayo Gekul, wakati nafasi ya umakamu bara  inagombewa na  Elizabeth Kasera, Esther Fulano, Moza Ally, Francis Garatwa, Mohonia Mwita.

Kwa upande wa Zanzibar, wanaogombea nafasi hiyo ni Rukia Aboubakar Mohammed  na Omar Othman Nassoro.

Mkutano huo utakwenda sambamba na ule wa Baraza la Wazee la Chadema ambalo litafanya uchaguzi wa kumchagua mwenyekiti na makamu mwenyekiti wa bara na visiwani ambapo mgeni rasmi atakuwa Dk Azavel Lwaitama.