Bei ya nyama yapaa Geita

Muktasari:

Wafanyabiashara wa mifugo katika mnada wa Katoro uliopo wilayani Geita wamesema kupanda kwa bei ya nyama katika maeneo mbalimbali ya mji wa Geita kumetokana na kupanda kwa bei ya mifugo kulikosababishwa na uhaba wa ng’ombe.

Geita. Wafanyabiashara wa mifugo katika mnada wa Katoro uliopo wilayani Geita wamesema kupanda kwa bei ya nyama katika maeneo mbalimbali ya mji wa Geita kumetokana na kupanda kwa bei ya mifugo kulikosababishwa na uhaba wa ng’ombe.

Wakizungumza kwa nyakati leo Jumatatu Oktoba 19, 2020  wakati wa hafla ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa mnada wa mifugo utakaogharimu zaidi ya Sh365 milioni,  Lusoga Mganga na Lucas Katwika wamesema wengi wao waliuza mifugo yao kipindi cha nyuma kwa kukosa maeneo ya malisho.

“Baadhi ya mifugo iliuzwa nje ya mkoa wa Geita hali iliyosababisha uhaba wa mifugo ndani ya mkoa na hivyo kupandisha bei ya nyama kutoka Sh6, 000 hadi Sh7, 000,” alisema Mganga

Ili kukabiliana na changamoto ya kukosekana kwa soko la uhakika la mifugo, Halmashauri ya Geita inatekeleza mradi wa ujenzi wa mnada wa mifugo ambapo kaimu mkurugenzi halmashauri hiyo, Donald Nssoko amesema uamuzi huo sio tu utawahakikishia wafugaji soko, bali utaongeza mapato kupitia ushuru wa ndani.

Halmashauri hiyo inatekeleza mradi wa ujenzi wa soko la kisasa katika mji mdogo wa Katoro utakaokuwa na maduka 176 kwa gharama ya zaidi ya Sh4 bilioni.

Hadi sasa, tayari ujenzi wa jengo la ghorofa moja lenye maduka ya biashara 88 unaendelea kwa gharama ya zaidi ya Sh1.5 bilioni zinazotokana na fedha zinazotolewa na mgodi wa dhahabu wa Geita (GGM) kupitia mpango wa wajibu kwa jamii.