Bei ya petrol, dizeli yashuka

Dar es Salaam. Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) imetangaza kushuka kwa bei ya mafuta nchini itakayoanza kutumika leo Aprili Mosi.
Ewura imesema mabadiliko hayo yanatokana na mabadiliko ya bei za mafuta katika soko la dunia na gharama za usafirishaji.
Kwa Dar es Salaam bei za rejareja petroli itauzwa Sh2,087 kutoka Sh2,204, dizeli Sh1,989 kutoka Sh2,153 na mafuta ya taa yatauzwa Sh1,923 kutoka 2,116 . Bei za jumla Ewura imesema petroli imeshuka Sh166, dizeli Sh164 na mafuta ya taa Sh 192.
Kadhalika bei imeshuka katika mikoa ya kaskazini Tanga, Kilimanjaro, Arusha na Manyara bei zimeshuka kwa petroli Sh 86, dizeli Sh 56 na mafuta ya taa 85.
Hata hivyo mikoa ya kusini Mtwara, Lindi na Ruvuma bei itakayotumika ni ya mwezi Machi kwakuwa hakuna mafuta yaliyopokelewa katika bandari ya Mtwara.
Ewura imesisitiza wananchi kutumia simu za mkononi kujua bei ya mafuta ya eneo husika walilopo kwa kupiga *152*00# na kufuata maelekezo.