Benki ya DCB yazindua akiba ya mpango wa elimu

Wednesday October 9 2019

By Ephrahim Bahemu, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Benki ya DCB imeanzisha akaunti maalum kwa ajili ya akiba ya mpango wa elimu ambayo inatoa uhakika wa kusoma kwa mtoto hata baada ya msomeshaji kufariki au kupata majanga yatakayosababisha ashindwe kutekeleza jukumu hilo.

Akaunti hiyo yenye mfumo kama wa bima, imezinduliwa leo Jumatano Oktoba 9, 2019 jijini hapa na katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Godfrey Ndalahwa amesema benki itanufaika kwa kuongeza amana na kuongeza idadi ya wateja watakaovutiwa na huduma hiyo.

“Leo tunazindua akaunti yetu iitwayo DCB Skonga, tunalenga kukuza elimu na hakuna masharti magumu katika akaunti hii. Kiasi kidogo cha mchango ni kuanzia Sh5,000 kwa mwezi, unaweza kupata mkopo hadi wa asilimia 50 ya amana zako na unaweza kutoa amana zako wakati wowote,” amesema Ndalahwa.

Ametaja faida nyingine kuwa akaunti hiyo,  mteja atapata bonasi kila mwaka inayolingana na mchango wake wa mwezi.

“Tulichokifanya ni ubunifu mzuri katika soko la fedha, tunashirikiana na watu wa bima (bila kuwataja), faida tunayoipata sisi ni kuongeza wateja na amana na unajua amana ndiyo roho ya benki, tunazitumia katika biashara kuzalisha fedha zaidi,” amesema Ndalahwa.

Mkurugenzi wa biashara wa benki hiyo, James Ngaluko amesema DCB inatoa fursa kwa wazazi na walezi kupanga namna ambavyo mtoto wao atasoma kuanzia ngazi yoyote hadi chuo kikuu.

Advertisement

“Endapo mzazi au mlezi atafariki au kupata ulemavu wa kudumu ambao utasababisha ashindwe kutimiza majukumu yake, kwanza atapewa amana zote ambazo alikuwa amewahi kuchangia na benki itachukua jukumu la kumsomesha mtoto kwa kulipa fedha ambazo ni sawa na michango ya akaunti yake kila mwaka hivyo mzazi ndiye wa kupanga mwanae anufaike vipi,” amesema.

Amesema kama mtoto atafariki dunia, mchangiaji atapatiwa amana zake zote au anaweza kuzihamishia kwa mtoto mwingine, lakini pia kinapotokea kifo benki hutoa ubani.


Advertisement