Benki ya Dunia yaipongeza Serikali ya Tanzania inavyoboresha elimu

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Dunia ukanda wa nchi za Afrika, Anne Kabagambe

Muktasari:

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Dunia (WB) ukanda wa nchi za Afrika, Anne Kabagambe akiwa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa wa Tanzania, Joyce Ndalichako wameitembelea shule ya Sekondari Kibasila jijini Dar es Salaam ambapo WB  imeipongeza Serikali ya Tanzania kwa kuhakikisha watoto wenye umri wa kwenda shule wanapata nafasi hiyo.

Dar es Salaam. Benki ya Dunia (WB) imepongeza Serikali ya Tanzania kwa kutoa kipaumbele kwa sekta ya elimu nchini humo kwa jinsi inavyohakikisha watoto wenye umri wa kwenda shule wanapata nafasi hiyo.

Pongezi hizo zilitolewa jana Alhamisi Agosti 22,2019 jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Dunia ukanda wa nchi za Afrika, Anne Kabagambe mara alipofanya ziara katika shule ya Sekondari Kibasila akiwa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa, Joyce Ndalichako.

Kabagambe alitembelea shule hiyo kwa sababu Benki ya Dunia inaendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika juhudi zinazofanywa kwenye sekta ya elimu ikitambua elimu ni ndio chimbuko la maendeleo katika mchi yoyote.

Kwa upande wake, Waziri Ndalichako alisema Benki ya Dunia imekuwa ikishirikiana na Serikali katika miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo mradi wa elimu unaojulika kama Lipa Kulingana na Matokeo (EP4R) ambapo WB imetoa dola za kimarekani milioni 202 katika mradi huo ulioanza kutekelezwa mwaka 2014 na unategemewa kumalizika mwaka 2021.

Alisema kupitia mradi huo takribani Sh141 bilioni zimeshatumika kwa ajili ya kukarabati shule kongwe 62, kujenga vyumba vya madarasa 2,876, matundu ya vyoo 6,558, nyumba za walimu 59, mabwalo 76, majengo ya utawala 16, mabweni 533 kwa ajili ya kuwaepusha watoto wa kike na changamoto za mbalimbali, pamoja na kujenga mifumo ya maji safi kwenye baadhi ya shule ambazo hazikuwa na vyanzo vya maji.

Waziri Ndalichako alisema kwa upande wa Shule ya Sekondari Kibasila  Sh900 milioni zimetengwa kwenye bajeti ya mwaka wa fedha 2019/2020  kwa ajili ya ukarabati na tayari wataalamu wameanza kufanya tathmini ya majengo ya shule hiyo ambayo ukarabati wake utaanza wakati wowote kuanzia sasa.

Awali, Mkuu wa Shule hiyo, Yasinta Matilya alisema moja ya changamoto inayokabili shule hiyo ni utoro wa wanafunzi unaotokana na changamoto za kifamilia ikiwemo watoto kulelewa na mzazi mmoja, kipato duni, umbali wa makazi ya wanafunzi.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wanafunzi wa shule hiyo waliiomba Serikali kuwapatia walimu wa saikolojia watakaowasaidia kujitambua ikiwa ni pamoja na kuwajengea mabweni ili kuepukana na vishawishi vya barabarani pamoja na usumbufu wa usafiri wa unaopelekea wanafunzi kuacha shule.