Benki ya NBC yatoa somo kwa wateja wake

Sunday September 15 2019

By Mwandishi wetu, Mwananchi [email protected]

Dodoma. Benki ya NBC imefanya kongamano maalum la kibiashara kwa ajili ya wateja wake wadogo na wakati jijini Dodoma nchini Tanzania ambalo pamoja na mambo mengine lililenga kuwaongezea wateja hao uelewa kuhusiana na mabadiliko ya kihuduma na fursa za kiuwezeshaji kutoka benki hiyo.

Katika kongamano hilo  mbali na masuala ya kibenki washiriki walipata fursa ya kusikiliza na kuchangia mada kutoka kwa wawakilishi wa taasisi nyingine ikiwemo Chemba ya biashara, viwanda na kilimo (TCCIA) na  Baraza la Uwezeshaji la Taifa (NEEC) ambao walielezea fursa mbalimbali za kibiashara ndani na nje ya Tanzania ikiwemo nafasi ya taasisi hizo katika kuwaunganisha wafanyabiashara na wenzao kutoka nje ya nchi.

Akizungumza wakati wa kongamano hilo lililofanyika jijini Dodoma hivi karibuni, Meneja Ukuzaji wa Biashara Kitengo cha biashara ndogondogo na za kati wa Benki  hiyo,  Jonathan Bitababaje alisema kufuatia uboreshwaji mkubwa wa huduma za benki hiyo ambazo zinaendana na kasi ya kiteknolojia na fursa za kiuchumi kumekuwa na hitaji kubwa kwa wateja kujengewa uelewa ili waweze kwenda sambamba na mabadiliko hayo.

“NBC kwa sasa tumefanya mabadiliko makubwa ya kihuduma yanayoendana na kasi ya kiteknolojia na ukuaji wa uchumi na tumeona mabadiliko haya yatakuwa na tija zaidi kwa wateja wetu hasa wadogo na wakati  ikiwa tu tutawajengea uelewa wa kutosha ili waweze kwenda sambamba mabadiliko haya badala ya kuwa changamoto,’’ alibainisha.

Alisema mbali na kuwajengea uelewa kuhusu huduma za benki hiyo, kupitia kongamano hilo washiriki waliweza kutoa maoni yao ikiwa ni mrejesho wa huduma wanazopata kutoka benki hiyo, hatua aliyosema itasaidia taasisi  hiyo kuboresha zaidi huduma hizo sambamba na kubuni huduma mpya zinazoendana na mahitaji ya wateja hao.

Advertisement