Bibi mzee wa miaka 70 auawa nyumbani kwake

Muktasari:

Mwanamke mwenye umri wa miaka 70 aliyetambulika kwa jina la Albetina Pius mkazi wa Mlimba wilayani Kilombero, amekutwa amekufa nyumbani kwake huku mwili wake ukiwa na majeraha na mdomoni ukitokwa mapovu na damu.

Morogoro/Manyara. Mwanamke mwenye umri wa miaka 70 aliyetambulika kwa jina la Albetina Pius mkazi wa Mlimba wilayani Kilombero, amekutwa amekufa nyumbani kwake huku mwili wake ukiwa na majeraha na mdomoni ukitokwa mapovu na damu.

Polisi wamesema wanachunguza kifo hicho kwa kuchunguza majereha ya bibi huyo ili kubaini aina ya silaha iliyotumika katika mauaji hayo.

Kamanda wa polisi wa mkoa, Wilbrod Mutafungwa alisema tukio hilo lilitokea usiku wa Novemba 27 na watuhumiwa wa mauaji hayo hawajapatikana na polisi wanaendelea kuwasaka.

Alisema kabla ya kufanya mauaji hayo watuhumiwa walipasua taa ya umeme iliyokuwa kwenye mlango wa nyuma wa nyumba ya bibi huyo ili wasionekane wakati wa kufanya mauaji hayo.

Kamanda Mutafungwa alisema baada ya kupasua taa walivunja mlango na kuingia ndani na kufanya mauaji hayo bila ya kuiba mali yoyote ya bibi huyo ambaye alikuwa akiishi peke yake.

Alisema kuwa polisi walipofika eneo la tukio walikuta nguo za kiume zilizoachwa na watuhumiwa wa mauaji hayo ambazo walizichukua ili ziwasaidie katika uchunguzi wa tukio hilo.

Katika kilichoonekana kulihusisha tukio hilo na ushirikiana, Kamanda Mutafungwa aliwataka wananchi kuachana na imani za kishirikina na kulisaidia jeshi la polisi kutoa taarifa zitakazofanikisha kukamatwa kwa wahusika wa mauaji ya bibi huyo ili wachukuliwe hatua za kisheria.

Katika tukio jingine, mkazi wa Babati mkoani Manyara, Nicodemu Panga amejinyonga hadi kufa kwa kutumia kanga na kuzikwa juzi.

Mkuu wa upelelezi na makosa ya jinai wa mkoa wa Manyara, Joshua Mwafulango alisema Panga alifariki dunia kwa kujinyonga kwa kanga Desemba 2.

Mwafulango alisema polisi wanaendelea na uchunguzi wa kifo hicho cha Panga ambaye alikuwa katibu wa CCM tawi la Tsaayo kata ya Arr ila uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa chanzo cha Panga kujiua ni matatizo ya kifamilia.

Mmoja wa majirani wa eneo hilo, John Humay alisema Panga alikuwa na mgogoro wa kifamilia na mke wake ambaye alikaa naye muda mrefu na kuzaa pamoja watoto sita ila mtoto mmoja alifariki.

Humay alisema baada ya kukaa muda mrefu na mkewe walitengana wakawa kwenye vikao vya mara kwa mara vya kuwapatanisha.

“Maisha yake yalianza kuyumba hivi karibuni baada ya kuona anaishi bila mwenza wake ndipo akaamua kujinyonga kwa kutumia kanga na kufariki dunia,” alisema.