Bila barakoa hakuna kuingia KCMC

Wednesday April 15 2020
pic barakoa

Moshi. Uongozi wa Hospitali ya Rufaa ya KCMC umetangaza utaratibu mpya wa wagonjwa na ndugu kuingia hospitali hapo wakitakiwa kuvaa barakoa.

Utaratibu huo ulianza kutumika kwa wafanyakazi wa kada zote hospitalini hapo  jana Aprili 14, 2020 na leo Aprili 15, 2020 umeanza kutumika  kwa watu wote iwe ni kwa mgonjwa au ndugu wa mgonjwa.

Ofisa Habari wa hospitali hiyo inayomilikiwa na Shirika la Msamaria Mwema (GSF), Gabrie Chisseo amesema wamechukua hatua hiyo ili kujikinga na homa ya mapafu inayosababishwa na virusi vya corona.

“Kuanzia sasa hatutaruhusu mgonjwa, mteja au ndugu wa mgonjwa kuingia katika maeneo ya hospitali bila kuvaa barakoa (mask). Hii ni lazima ili uingie kupata huduma ni lazima uzingatie maagizo hayo,” amesema.

Kwa mujibu wa Chisseo, wameamua kuweka katazo hilo kwa kuwa wanathamini wagonjwa na watoa huduma na kwamba ni lazima waendelee kutoa huduma zote za afya bila kubagua huku wakichukua tahadhari.

“Tuwaombe wateja wetu wote uwe ni mgonjwa, ndugu wa mgonjwa au ni mteja wetu kuwa wavumilivu katika kipindi hiki kigumu ambacho sekta ya afya inakipitia kutokana na ugonjwa unaosababishwa na virusi vya corona,” amesisitiza.

Advertisement

Uongozi wa KCMC umechukua uamuzi huo ikiwa ni siku moja tu baada ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kueleza kuwa watu hadi kufikia Aprili 14,2020 walioambukizwa ugonjwa huo walikuwa wamefikia 53 Tanzania Bara na Zanzibar.

Lakini leo Aprili 15,2020, Waziri wa Afya wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Hamad Rashid Mohamed ametangaza ongezeko la wagonjwa wapya 6 walioambukizwa virusi hivyo.

Advertisement