Bilionea wa Tanzania Ali Mufuruki amefariki dunia

Muktasari:

  • Mfanyabiashara Ali Mufuruki amefariki leo alfajiri alipokuwa akipatiwa matibabu nchini Afrika Kusini

Dar es Salaam. Mfanyabiashara Ali Mufuruki  (60) amefariki dunia leo nchini Afrika Kusini alikokuwa akipatiwa matibabu.

Mufuruki ambaye ni mwenyekiti mwanzilishi wa Jukwaa la maofisa watendaji wakuu wa  kampuni (Ceo roundtable) amekutwa na umauti akiwa na familia yake.

Mufuruki ni kati ya matajiri wakubwa 10 wa Tanzania akiwa ni mmiliki wa Kampuni ya Infotech Investment Group Limited na maduka ya Wolworth.

Oktoba 18, 2019 Mufuruki alijiuzulu nafasi yake ya  Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Kampuni ya Vodacom Tanzania ili kupata muda zaidi wa kuendelea na biashara zake.

Mwenyekiti wa sasa wa Ceort, Sanjay Rughan amethibitisha kutokea kwa kifo hicho kilichotokea saa tisa alfajiri katika Hospitali ya Morningside.

Sanjay amesema awali, Mufuruki alikuwa amelazwa katika Hospitali ya Agakhan na hali yake ilibadilika jana ndipo alipopelekwa Afrika Kusini.

Kwa mujibu wa Sanjar mfanyabiashara huyo alikuwa akisumbuliwa na  ugonjwa wa homa ya mapafu.

SOMA ZAIDI