Binti abakwa mpaka kufa, mwili watelekezwa shamba la mahindi

Muktasari:

Watu wasiojulikana Mkoa wa Katavi wamemwingilia kimwili kwa nguvu binti wa miaka 22 hadi kumsababishia kifo.

Katavi. Msichana wa miaka 22, Jenipha Isaya   mkazi wa mtaa wa Kazima Manispaa ya Mpanda mkoani Katavi nchini Tanzania  amefariki dunia baada ya kuingiliwa kimwili kwa nguvu, kisha  mwili wake kutelekezwa kwenye shamba la mahindi lililo karibu na makazi ya watu.

Tukio hilo limetokea Alhamisi iliyopita ya Januari 23, 2020 baada ya wanafunzi wa shule ya msingi nyerere kupita eneo hilo wakati wakitoka shuleni na kuuona mwili wa Jenipha ukiwa umetelekezwa.

Akizungumza na Mwananchi  baba wa marehemu Isaya Shabani alisema alipokea taarifa hizo kwa njia ya simu majira ya saa 7:00 mchana na  kuambiwa mwanaye amefariki kwa kifo  cha kutatanisha bila  wahusika kufahamika.

"Mimi nakaa Kanoge nilishatengana na mke wangu, nilipopata taarifa nilikuja na kuelezwa amekutwa kando ya barabara karibu na shule ya msingi Nyerere amefanyiwa vitendo hivyo na wahusika hawafahamiki, lakini mwili wake ulikuwa umechukuliwa na polisi," alisema Shabani akaongeza.

"Walisema tunatakiwa kwenda polisi kutoa maelezo asubuhi, kweli tulifika polisi na kutoa maelezo baadaye wakaruhusu kwenda kuchukua mwili hospitalini."

Mwenyekiti wa serikali ya mtaa wa Kazima, Flaviana Salala alisema  alipata taarifa hizo  kwa dereva wa bodaboda saa 6:00 kisha kufika eneo la tukio na kukuta marehemu akiwa utupu huku amewekewa tofali kiunoni kisha miguu yake kukunjwa.

"Nilimtambua marehemu alikuwa anaishi na mama yake katika mtaa wangu na ni tukio la kwanza kutokea, nimelipokea kwa masikitiko makubwa ni  la kinyama na linasikitisha," alisema Salala.

Mratibu wa tiba hospitali ya Mkoa wa Katavi, Frank Elisha amekiri  kupokea mwili wa marehemu na baada ya kufanya uchunguzi wa kitabibu  inasadikika ni kweli alifanyiwa vitendo hivyo vya kikatili.

"Ni kweli inasadikika aliingiliwa kwa nguvu kwenye maeneo yake ya Siri," alisema Elisha.

Hili ni tukio la pili kutokea kwa mwezi huu likiwamo  la mtoto mwenye umri wa miaka 10 kunajisiwa hadi kufa baada ya kwenda  kuchota maji na mwenzake.