Biteko amweka kwenye wakati mgumu mkurugenzi wa Indiana

Viongozi wa Wizara ya Madini wakiwa kwenye kikao cha Waziri wa Madini, Doto Biteko aliyeshika kidevu na Mkurugenzi wa Kampuni ya Indiana, Bob Adam kushoto kwa waziri leo ofisini kwake Jijini Dodoma. Kutoka kulia kwa waziri ni Mkurugenzi wa Sera na Mipango Augustine Ollal, Mkurugenzi wa huduma za sheria Edwin Igenge na Kamishna msaidizi, Terence Ngole. Na ofisi ya WM.

 

Muktasari:

  • Biteko akutana na kufanya mazungumzo na mkurugenzi kampuni ya Indiana akitaka aelezwe kwa kina kuhusu kampuni kufanya makubaliano na Ngwena bila kuitarifu wizara hiyo

Dar es Salaam. Waziri wa Madini, Dotto Biteko amekutana na mkurugenzi wa Kampuni ya Indiana, Bob Adam ili kujadili ushirika wao na kampuni ya Ngwena Ltd ambao wizara hiyo  haiutambui.

Hatua ya Biteko kukutana na Adam imekuja baada ya waziri huyo kufanya ziara wiki iliyopita wilayani Nachingwea mkoani Lindi na kubaini kuunganishwa kwa  Ngwena Ltd na Indiana bila wizara hiyo kutaarifiwa.

Taarifa iliyotolewa jana Jumatatu Agosti20,2019 na wizara hiyo imeeleza Biteko  na Adam walikutana Jijini Dodoma .

Katika taarifa hiyo inaeleza kuwa Biteko amembana Adam kwa hoja zilizosababisha kutopatikana kwa majibu ya moja kwa moja kwa kile kilichodaiwa kutokukuwepo kwa uongozi wa kampuni ya Ngwena Ltd.

Biteko alitaka kufahamu kwa nini Ngwena na Indiana wamefanya makubaliano bila kutoa taarifa wizarani wakati kampuni moja ni ya Kitanzania nyingine ya kigeni, jambo jingine alitaka kuona makubaliano yenye faida kwa pande zote mbili  na kujua Serikali itanufaikaje.

“Hoja nyingine kwa nini kampuni husika zinatunzaje shehena kubwa ya sampuli za madini bila kuijulisha Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini (GST), ambayo ina dhamana ya utunzaji? Alihoji Biteko katika mazungumzo hayo.

Taarifa hiyo ilizidi kueleza kuwa Biteko aliendelea kumbana Adam kwa kumuuliza uhusika wake kwenye kampuni ya Ngwena Ltd, huku mkurugenzi wa huduma za sheria za Wizara ya Madini, Edwin Igenge akimhoji walianza lini ushirika huo, ilikuwa kabla au baada ya marekebisho ya Sheria ya mwaka 2017.

Akijibu maswali , Adam amesema Indiana ndiyo inayomiliki Ngwena Ltd na kufadhili kifedha na masuala mengine.

Kuhusu kabla au baada ya marekebisho ya sheria ya 2017, mkurugenzi huyo hakuwa na majibu ya moja kwa moja badala yake aliomba arejee kwenye nyaraka ili  kujiridhisha

 “Kampuni yetu ndiyo inayo miliki Ngwena Ltd kwa maana Indiana inamiliki asilimia 60 ya hisa zote na ndiyo maana ninasema Indiana inamiliki Ngwena,” amesema Adam.

Kutokana na  hali hiyo, Waziri Biteko ameagiza kupangwa kwa tarehe nyingine ya kukutana huku akimtaka Adam kurudi tena nchini  akiwa na uongozi wa Ngwena Ltd ili kufahamu kiundani kuhusu  makubaliano yao kwa kuwa hadi sasa  kampuni inayotambuliwa na Wizara ni Ngwena Ltd na siyo Indiana.