Biteko ang’aka mishahara ya Watanzania migodini

Waziri wa Madini Doto Biteko katikati akiwa kwenye kikao na uongozi wa mgodi wa dhahabu wa Geita (GGM) wakati wa ziara yake mgodini hapo. Kulia kwake ni Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhandisi Robert Gabriel, Mkuu wa Wilaya ya Geita, Joseph Maganga na kushoto kwa waziri ni Mkurugenzi Mtendaji wa GGM Richard Jordonson.

Muktasari:

Waziri wa Madini wa Tanzania, Dotto Biteko ameuagiza uongozi wa GGM kuwasilisha orodha ya malipo ya mishahara ya wafanyakazi wote kwa Kamishna wa Madini, Mhandisi David Mulabwa wiki ijayo.

Geita. Waziri wa Madini Doto Biteko pamoja na kuupongeza uongozi wa mgodi wa dhahabu wa Geita “GGM” katika  mambo mengi leo tarehe 16/11/2019 alikuwa “mbogo” kwa uongozi huo kuhusu suala la mishahara wanayolipwa Watanzania ambapo amebaini kutokuwepo kwa usawa.

Biteko amesema anaumia kuona Watanzania wakilipwa mishahara midogo ikilinganishwa na wageni licha ya kulingana sifa, ujuzi na elimu.

Amesema wakati mwingine utakuta Mtanzania anakuwa na sifa zaidi kuliko mgeni, lakini bado mzawa utakuta analipwa kiduchu ukilinganisha na mgeni.

Kutokana na hali hiyo, Waziri Biteko ameuagiza uongozi wa GGM kuwasilisha orodha ya malipo ya mishahara ya wafanyakazi wote kwa Kamishna wa Madini, Mhandisi David Mulabwa wiki ijayo.

Waziri huyo alianza kuhoji idadi ya idara zilizopo na zinaongozwa na akina nani huku akiuliza kuna watu wangapi wa kigeni katika idara hizo na majukumu yako.

“Sheria ya Mhasa sheria ya Local content inatoa mwongozo ni namna gani na wakati gani mgodi unaweza kumuajiri mtaalamu wa fani fulani kutoka nje endapo hakuna Mtanzania wa kuweza kushika wadhifa huo,” amesema Biteko.

Ameyasema hayo alipokuwa akizungumza  na uongozi wa mgodi wa GGM mkoani Geita alipoutembelea jana Jumamosi Novemba 16, 2019.

Biteko ameifanya ziara hiyo maalumu kwa  lengo la kufuatilia na kukagua uendeshaji wa shughuli za mgodi sambamba na kuangalia utekelezaji wa malalamiko ya wananchi na malipo ya ushuru wa Halmashauri (Service Levy) ambayo mgodi unawajibika katika malipo hayo.

Aidha, Biteko amekwenda kujiridhishi katika masuala mbalimbali ambayo kamati maalumu aliyoiunda kwenda mgodini hapo kwa ajili ya kuangalia na kukagua ili ajiridhishe kabla ya kutoa idhini ya kuruhusu mgodi huo kuanza uchimbaji wa chini kwa chini kufuatia maombi ya mgodi huo kwa waziri.

Kwa mujibu wa kifungu cha 40 cha marekebisho ya Sheria ya Madini ya Mwaka 2017,  hairuhusu uchimbaji wa chini kwa chini kwa mwekezaji au mgodi mpaka apate idhini (kibali) ya waziri mwenye dhamana ya Madini.

Waziri Biteko alishaainisha mambo mengi ya kuzingatiwa na mgodi kabla hawajaruhusiwa.

Hivyo, jana aliendelea kusisitiza kauli yake ya mara kwa mara kuwa raslimali hizo ziwe neema kwa wananchi na si mateso.

Waziri Biteko alitoa kauli hiyo kwa mara nyingine jana baada ya kupokea malalamiko ya wananchi takribani 350 ambao makazi yao yalipitiwa na tetemeko wakati wa ulipuaji wa miamba mgodini hapo.

Hivyo, amesema hadi kufikia mwishoni mwa mwaka huu, ukurasa wa suala la malipo ya fidia ya suala hilo uwe umefungwa.

Amesema mtu yeyote mwenye malalamiko ayapeleke kwa Mkuu wa Wilaya Geita kuanzia kesho Jumatatu Novemba 18 hadi 23, 2019.

Kwa upande wa uongozi wa mgodi ukiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji, Richard  Jordanson na Makamu Mkurugenzi Mtendaji, Simon Shayo kwa nyakati tofauti walitoa shukrani kwa ujio wa Waziri kwenye mgodi wao ikiwa ni mara yake ya kwanza kutembelea tangu alipoteuliwa kuwa Waziri wa Madini.

Wameongeza kuwa mgodi wao upo mstari wa mbele kutekeleza maagizo ya serikali na kwamba, wanapenda wawe wa kwanza kuchangia sehemu kubwa itakayo changia pato (GDP) la Taifa kwa upande wa madini.

Shayo amemwambia waziri kuwa mambo mengi aliyoyasema kama ya mpango wa ufukiaji mashimo baada ya mgodi kufungwa, ulipaji wa ushuru wa Halmashauri za wilaya, ulipaji fidia kwa wananchi wataendelea kutekeleza.

Akiwa kwenye mgodi wa RZ unaomilikiwa na mwekezaji kutoka China anae fahamika kwa jina la Lyuu,  amemtaka mwekezaji huyo kufanya kazi zake kwa kuzingatia sheria na utoaji wa mikataba ya ajira na makato ya NSSF kwa wafanyakazi wake na kuiwasilisha kwa mamlaka husika.