Biteko awapa somo watumishi wapya Tume ya Madini

Wednesday December 4 2019

By Sharon Sauwa, Mwananchi [email protected]

Dodoma. Waziri wa Madini nchini Tanzania, Dotto Biteko amewafunda watumishi wapya 116 walioajiriwa na Tume ya Madini nchini akiwataka kuacha tamaa, kufanya kazi kwa kufuata sheria na kanuni.

Biteko ameyasema hayo leo Jumatano Desemba 4,  2019 wakati akizungumza na watumishi wa tume hiyo mjini Dodoma.

Amesema sio watu wote wanaofanya kazi sekta ya madini ni matajiri  kama inavyoaminika na watu wengi.

“Tahadhari aliyoitoa Katibu Mkuu (Katibu Mkuu Wizara ya Madini Profesa, Simon Msanjila) muache tamaa ni tahadhari ya kufanyiwa kazi. Tuliondoa watu  zaidi ya 100 kwa sababu ya rekodi ya mahusiano,” amesema.

Amewataka kuwa wapambanaji na kufanya kazi zao kwa kufuata sheria pamoja na kanuni ili  kuonyesha matokeo badala ya kuwa wanung’unikaji.

“Mungu anashughulika na watu wasionung’unika. Sekta ya madini anayenung’unika hawezi dumu,” amesema.

Advertisement

Amewataka watumishi hao kuwasaidia viongozi watakaowakuta katika maeneo yao ya kazi badala ya kugombana nao.

Biteko amesema endapo watagombana nao wataishi maisha yasiyo na furaha yatakayosababisha walalamikiwe.

“Jifunzeni kujishusha it pays very much (inalipa sana) kuwa mkimya ukajishusha kuliko kuwa mwongeaji wakati wote,” amesema.

Biteko amesema watumishi hao waelewe kuwa wanaenda kufanya kazi na watu wanaoongea zaidi na majungu.

“Kama mimi ningekuwa nafanyia kazi kila ujumbe mfupi wa maneno ninaotumiwa kusingekuwa na mtumishi ambaye angebaki,” amesema.

Advertisement