BoT yabadili alama za noti kuondoa zilizochakaa

Dar es Salaam. Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imetangazwa kuingiza noti zenye alama mpya za utambuzi kwenye mzunguko wa fedha, ili kuondoa zilizochakaa.

Miongoni mwa alama zilizowekwa kwenye noti hizo za shilingi 1,000, 2,000, 5,000 na 10,000 ni sahihi ya waziri wa fedha wa sasa Dk Philip Mpango na ile ya gavana wa BoT, Profesa Florens Luoga.

Taarifa ya BoT kwa benki na taasisi za kifedha iliyotolewa Aprili 2 inaeleza kuwa badiliko la msingi ni uzi mwembamba katika noti hizo na kuwa alama nyingine zitaendelea kama ilivyo katika noti za toleo la 2010.

“Kazi ya Benki Kuu ni kuhakikisha kunakuwa na fedha za kutosha kufanya manunuzi katika mzunguko wa fedha na fedha hizo zinapitia mazingira tofauti hivyo huchakaa na zikichakaa lazima zitengenezwe nyingine,” alisema Mkurugenzi wa huduma za benki wa BoT, Agustino Hotay.

“Kadri noti inavyokaa kwenye mzunguko watu wanaanza kujaribu kughushi, utakumbuka mwaka jana mwishoni fedha nyingi bandia zilikamatwa. Nasi tunapopata fursa ya kuchapisha fedha mpya tunaimarisha na alama za usalama ili kudhibiti wanaoghushi,” alisema.

Hotay, alisema noti hizo mpya na zile zilizokuwepo katika mzunguko zitaendelea kutumika kama kawaida na fedha ambazo zitakuwa zikichakaa zitakuwa zinaondolewa katika mzunguko.

Mtaalamu wa uchumi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Abel Kinyondo alisema hatua hiyo haina athari zozote kwa uchumi kwani fedha inayowekwa kwenye mzunguko inarudishiwa iliyoondoshwa.

“Kama kuna taharuki ni watu kushindwa kuelewa kilichofanyika lakini kimsingi hakina athari yoyote kiuchumi hali ingestua kama fedha zingeongezwa tu katika mzunguko bila sababu yoyote lakini kilichofanyika sasa ni kurudishia kilichokuwepo,” alisema Kinyondo.