Bomba la gesi Songas latengamaa

Muktasari:

Baada ya kutokea kwa hitilafu ya uvujaji wa gesi juzi katika kituo cha Songas Kilwa imeelezwa mafundi wanaendelea na matengenezo na kwamba usiku wa leo kituo cha Songas Ubungo kitaanza kupokea gesi.

Kilwa. Baada ya marekebisho ya siku tatu mfululizo, Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) limesema gesi asilia kutoka Somanga mkoani Mtwara itaanza kufika Ubungo kwa kiwango cha kutosha hivyo kurejesha ufuaji kama ilivyokuwa awali.

Kutokana na juhudi zilizochukuliwa na wataalamu, Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco, Dk Tito Mwinuka akizungumza na Mwananchi, leo Jumanne Novemba 5, 2019 amesema mpaka usiku wa jana walitarajia kila kitu kingeenda sawa.

“Gesi imeshaanza kufika japo kwa kiasi kidogo lakini mpaka usiku wa leo itaongezeka na kukidhi mahitaji ya uzalishaji,” amesema Dk Mwinuka.

Kutengamaa kwa bomba hilo linalosafirisha gesi inayotumika kwenye mitambo ya kufua umeme ya kampuni ya Songas iliyopo Ubungo kutarudisha uhakika wa upatikanaji wa nishati hiyo kwa wananchi wa maeneo yaliyotangazwa kwamba yangekuwa na katizo la umeme kwa vipindi tofauti.

 Bomba la gesi la kampuni hiyo lilipata hitilafu jioni ya Novemba 3, baada ya gesi kuvuja kwenye moja ya valvu zake hivyo kuzua taharuki kwa wananchi wa Kijiji cha Somangafungu kilichopo Kilwa mkoani Lindi.

Kutokana na hali hiyo, wataalamu walilazimika kuzima mitambo ya kufua gesi hiyo iliyopo katika Kijiji cha Songosongo na kuchukua hatua za kiusalama kurekebisha tatizo lililotokea.

“Wametuhakikishia kazi ya kurudishia mitambo itakamilika leo usiku na baadaye wataanza kujaza gesi. Kwa sababu ni  kubwa na refu itachukua hadi saa sita gesi ifike Dar es Salaam,” alisema Dk Mwinuka.

Kutokana na kukosekana kwa gesi kituo cha kufua umeme cha Songas kilichopo Ubungo kilizimwa tangu juzi hivyo kupunguza upatikanaji w anishati hiyo katika mikoa ya Dar es Salaam na Pwani pamoja na Zanzibar.

Kwa juhudi zilizofanyika, amesema mitambo miwili ya Songas inafanya kazi na mpaka usiku mitambo yote itakuwa inafanyakazi  hivyo kumaliza upungufu uliokuwapo.

Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Songas, Nigel Whittaker kuhusu tukio hilo ilifafanua kuwa uvujaji huo ulitokea wakati wataalamu wake wakilikarabati bomba hilo tangu wiki tatu zilizopita.

“Songas inachunguza kubaini chanzo cha kizuizi kushindwa kuhimili ili kuchukua hatua itakapobidi. Kwa sasa kampuni inafanya kazi ya ziada kuhakikisha inarudisha bomba katika hali yake ya kawaida ndani ya siku mbili zijazo,” alisema Whittaker.