VIDEO: Bomba la gesi lazua taharuki Kilwa

Muktasari:

  • Gesi inayovuja kwenye bomba la gesi linalomilikiwa na kampuni ya Songas na kutoa mungurumo na moshi mkubwa imesimamisha shughuli za usafiri wilayani hapa kutokana na watu kuhofia usalama wao.

Kilwa. Shughuli zimesimama kwa muda wilayani hapa baada ya bomba la gesi asilia kuvujisha nishati hiyo katika kituo cha kupokea gesi cha Songas eneo la Songosongo na kusababisha muungurumo na moshi mkubwa uliowatisha wananchi.

Kutokana na hali hiyo magari yaliyokuwa yanayopita eneo hili yamelazimika kusimama huku ulinzi ukiimarishwa eneo la tukio kuzuia madhara yanayoweza kujitokeza.

Gesi hiyo inayovuja kwenye kituo hicho kinachomilikiwa na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) hivyo kuwashawishi walinzi wa kituo jirani cha kupokea gesi kutoka Madimba Mtwara na Songosongo kilicho chini ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) wakisaidia kuimarisha ulinzi.

“Ni kweli kuna hitilafu kidogo. Wataalamu wetu wanashughulikia hali hiyo ila hakuna moto wala madhara yoyote kwa binadamu,” amesema Nigel Whittaker mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya Songas. 

Mkurugenzi huyo amesema walichofanya mpaka sasa ni kusimamisha uzalishaji wa gesi hiyo ili kurekebisha tatizo lililopo.

Kusaidia kudhibiti hali hiyo, gari la kikosi cha Zimamoto na Uokoaji limefika eneo la tukio lakini halifanyi chochote. Wananchi wapo kando wakishangaa kinachoendelea katika mradi huo.