Bombardier iliyoachiwa Canada kutua kesho Mwanza

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza John Mongella wa Pili Kulia akizungumza na waandishi wa Habari  ambapo amewataka wananchi wa Mkoa huo kujitokeza Desemba 14 katika uwanja wa Ndege wa Mwanza kwa ajili ya mapokezi ya Ndege aina ya Bombadier Q 400 iliyokuwa imeshikiliwa Nchini Canada. Picha na Johari Shani

Muktasari:

  • Rais wa Tanzania, John Magufuli kesho Jumamosi, atawaongoza Watanzania katika mapokezi ya ndege aina ya Bombardier Q400 iliyokuwa imekamatwa nchini Canada ambayo itawasili katika uwanja wa Ndege jijini Mwanza nchini humo.

Mwanza. Ndege ya Tanzania aina ya Bombardier Q400 iliyokuwa imekamatwa nchini Canada itawasili nchini humo kesho Jumamosi Desemba 14, 2019 katika Uwanja wa Ndege jijini Mwanza.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Ijumaa Desemba 13, 2019, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella amesema ndege hiyo itapokewa saa 10 jioni.

Amewaomba wananchi wa ndani na nje ya mkoa huo kujitokeza kwa wingi kushuhudia tukio hilo.

"Tukio hilo la kihistoria litaongozwa na Rais John Magufuli, tunawaomba wananchi kuwa wazalendo kufika kwa wingi uwanja wa ndege saa 8 mchana, utakuwapo utaratibu wa wananchi wote kupata fursa ya kuingia," amesema Mongella

Ndege hiyo ilikuwa inashikiliwa nchini Canada baada ya mkulima Hermanus Steyn, raia wa Afrika Kusini ambaye alifungua kesi ya madai akidai fidia ya dola 33 milioni.

Jana Alhamisi Desemba 12, 2019, akifungua mkutano wa Halmashauri Kuu ya chama tawala cha CCM jijini Mwanza alisema, “ndege yetu iliyokuwa inashikiliwa Canada imeachiliwa, wananchi watatangaziwa tarehe ya kuwasili ili wakaipokea na tutaipokelea hapa Mwanza.”

Steyn, anadai fidia baada ya mali zake kutaifishwa na Serikali ya Tanzania mwaka 1980. Hata hivyo, Septemba 3, 2019 mahakama hiyo iliamuru ndege hiyo iliyokuwa imezuiwa katika uwanja wa ndege wa Oliver Tambo kuachiwa baada ya Serikali kushinda kesi bila kutoa fedha yoyote.