Bondia Mike Tyson anunua ekari 40 za kulimia bangi

Muktasari:

Bondia maarufu Duniani, Mike Tyson yuko mbioni kuzalisha biashara ya bangi huku akibainisha huvuta hadi tani 10 kwa mwezi

Dar es Salaam. Bondia maarufu Duniani, Mike Tyson (53) yuko mbioni kuanzisha biashara ya bangi na tayari ameshanunua ekari 40 kwa ajili ya kuzalisha bidhaa hiyo katika Jiji la California.

Mbali na kuanzisha biashara hiyo pia amebainisha yeye binafsi huwa anatumia Sh91 milioni kununua bangi huku akiweka wazi kuwa huvuta hadi tani 10 za bangi kwa mwezi.

Bondia huyo alistaafu mchezo wa ngumi mwaka 2005, lakini baadaye aliamua kuwa mtangazaji wa kipindi cha “Hotboxin with Mike Tyson” akiwa na mwenzie Britton.

Tyson amesema anaamini biashara hiyo itafanya vizuri kuliko biashara yake ya awali kwani alitangazwa kufilisika mnamo 2003 licha ya kupata fedha nyingi wakati wa kazi yake ya ndondi.

“Tumeshawekeza kiasi cha bilioni moja katika kukuza, kuzalisha, kusambaza kutangaza biashara hiyo  na lengo langu ni kuelimisha umma juu ya uwezo wa zao hilo katika kuponya baadhi ya magonjwa,” amesema Tyson

Mwaka 2016 alianzisha kampuni yake iitwayo Tyson Holistic Holdings ambayo ndiyo imetoa ramani na mpango wa shamba la bangi lililokamilika.