Boris agoma kuitisha Bunge la dharura

Waziri Mkuu wa Uingereza, Boris Johnson

Muktasari:

  • Jumapili iliyopita kiongozi wa chama kikuu cha upinzani cha Labour, Jeremy Corby alitoa pendekezo hilo baada ya kuvuja kwa ripoti ya Serikali inayotahadharisha juu ya kutokea uhaba wa chakula na dawa ikiwa nchi hiyo itajiondoa Brexit.

London, Uingereza. Waziri Mkuu wa Uingereza, Boris Johnson amekataa wazo la kuitisha Bunge la dharura ili kujadili suala la nchi hiyo kujiondoa katika Umoja wa Ulaya (EU) maarufu Brexit.

Kwa mujibu wa Shirika la habari la BBC, wabunge wa nchi hiyo sasa wako katika mapumziko ya majira ya kiangazi.

Jumapili iliyopita kiongozi wa chama kikuu cha upinzani cha Labour, Jeremy Corby, alitoa pendekezo hilo baada ya kuvuja kwa ripoti ya Serikali inayotahadharisha juu ya kutokea uhaba wa chakula na dawa nchini Uingereza ikiwa nchi hiyo itajiondoa Umoja wa Ulaya bila ya mkataba ifikapo Oktoba 31.

Awali Spika John Bercow alisema atahakikisha anamwekea vikwazo waziri mkuu huyo endapo kiongozi huyo atajaribu kulikwepa Bunge ili kukidhi mipango yake ya kuiondoa Uingereza katika Brexit.

Gazeti la The Telegraph la Uingereza lilimnukuu spika huyo akisema kuwa anazingatia kwa dhati haki ya Bunge kuwa na kauli katika mchakato huo.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliokuwa ukifanyika katika mji wa Edinburgh, Scotland, Spika Bercow alisema “ntapambana dhidi ya jaribio lolote la kulikwepa Bunge au kulifunga kwa malengo ya kutekeleza mpango wa Brexit.”

Kauli ya Spika Bercow inafuatia kauli ya Waziri Mkuu Boris kuwa atahakikisha Uingereza inajitoa Brexit ifikapo Oktoba 31 hata bila ya makubaliano.

Ripoti hiyo iliyochapishwa kwenye gazeti la Sunday Times inatahadharisha juu ya kutokea uhaba katika bidhaa za dawa, chakula na maji safi.

Waziri kivuli wa fedha, John McDonell alisema kuwa Corbyn atakutana na wanasiasa wengine wiki ijayo kujadili suala hilo.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu Boris Johnson anatarajiwa kukutana na Kansela Angela Merkel wa Ujerumani na Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa ili kuujadili upya mkataba wa Brexit.