Boris asaka huruma za Ujerumani, Ufaransa

Muktasari:

Waziri Mkuu wa Uingereza, Boris Johnson ameanza ziara katika nchini Ujerumani na Ufaransa lengo ikiwa ni kushawishi mataifa hayo yakubaliane na mpango wake wa Brexit.


Berlin, Ujerumani. Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amekutana na Waziri Mkuu wa Uingereza, Boris Johnson na kujadili namna ya kusonga mbele na mchakato wan chi hiyo kujitoa katika Umoja wa Ulaya (EU) marufu Breixt.

Viongozi hao wamekutana leo Alhamisi Agosti 22 wakati Boris alipofanya ziara yake ya kwanza nchini Ujerumani tangu achaguliwe mwezi Julai, kuwa Waziri Mkuu mpya wa Uingereza.

Akizungumza katika ziara hiyo, Boris aliutaka Umoja wa huo kufungua upya majadiliano kuhusu Brexit ili kuepusha nchi yake kuondoka bila makubaliano ifikapo Oktoba 31.

Kwa upande wake Kansela Merkel alisema Ujerumani ingependa Uingereza iondoke kwa makubaliano ingawa imejiandaa hata bila makubaliano.

Alisema ingawa mpango wa mpaka wa Ireland una madhara makubwa na lazima uondolewe anaamini ndiyo tegemeo hadi muafaka bora upatikane.

Ziara ya Boris inafuatia hatua ya Umoja huo kutangaza kukataa madai ya waziri mkuu huyo kuondoa mpango wa kutokuwa na ukaguzi mpakani ili kufikia makubaliano ya Brexit. Pia anatarajia kuzulu nchini Ufaransa.

Kwa mujibu wa EU, kiongozi huyo wa Uingereza mpaka sasa hajatoa mbadala unaoweza kufanyakazi.

Jumanne iliyopita, Boris alimwandikia Rais wa Baraza la Umoja huo, Donald Tusk akisisitiza kwamba Uingereza haiwezi kukubali kile inachoita hatua ya kutokuwa na ukaguzi mpakani ambayo ni kinyume na demokrasia, utaratibu ambao utaweza kuepukwa kati ya Ireland ambayo ni mwanachama wa Umoja huo na Ireland ya kaskazini ambayo ni sehemu ya Uingereza.

Tangu alipoingia madarakani mwezi uliopita, Boris amekuwa akisisitiza kwamba Uingereza itajitoa kutoka Umoja huo ifikapo Oktoba 31.

Kwa sasa waziri mkuu huyo ameongeza kasi ya matayarisho kwa ajili ya kujitoa bila makubaliano hali ambayo inaelezwa kwamba inasababisha mvurugiko mkubwa wa kiuchumi.