Boris ashangazwa wakurugenzi Thomas Cook kulipwa mamilioni

Muktasari:

Kwa sasa shirika hilo limesambaratika kutokana na mrundiko wa madeni yanayofikia dola bilioni 2.1.

London, Uingereza. Baada ya Shirika la Ndege la Uingereza, Thomas Cook kusambaratika na kuwaacha maelfu ya watu kuitegemea Serikali kuwarudisha nyumbani, Waziri Mkuu wa  nchi hiyo, Boris Johnson amehoji kwa nini wakuu wa shirika hilo walikuwa wakijilipa mishahara minono?

Shirika hilo ambalo pia husimamia hoteli, maeneo ya mapumziko na ndege kadhaa limekuwa likitoa huduma kwa wateja karibu milioni 19 kila mwaka huku zaidi ya 600,000 wakitoka katika nchi za nje.

Kwa sasa shirika hilo litahitaji msaada wa Serikali ya Uingereza pamoja na kampuni za bima kuwarudisha nyumbani watu hao.

Akizungumza mjini New York, Waziri Mkuu Boris alihoji kwa nini Taifa liachiwe mzigo na wakurugezi hao ambao waliamua kujilipa mamilioni ya fedha bila kuangalia athari zake.

Shirika la Thomas Cook limesambaratika kutokana na mrundiko wa madeni yanayofikia dola bilioni 2.1.

Hata hivyo, Serikali ya Uingereza imesema haitaki kujiingiza kwenye suala la shirika hilo na badala yake litatue matatizo yake.