Boris autega Umoja wa Ulaya

Waziri Mkuu wa Uingereza, Boris Johnson

Muktasari:

Adai hatolipa kiasi cha fedha ambazo nchi yake inastahili kuzitoa iwapo Umoja huo hautakubali mabadiliko katika mkataba ulioko.

London, Uingereza. Waziri Mkuu wa Uingereza, Boris Johnson amesema nchi yake haitalipa kiasi cha pauni bilioni 37 kwa ajili ya kujiondoa katika Umoja wa Ulaya (EU) maarufu Brexit iwapo hautakubali mabadiliko katika mkataba ulioko.

Kwa mujibu wa gazeti la The Mail la Uingereza, Boris alisema iwapo Uingereza itajiondoa katika Umoja huo bila ya mkataba wa kibiashara haitalipa fedha hizo.

Gazeti hilo liliandika kuwa mawakili wa Uingereza walisema badala yake Serikali hiyo italipa kiasi cha paundi bilioni tisa pekee.

Mawakili hao walisema pia kuwa hakutakuwa na gharama zinazohusiana na kipindi chochote cha mpito.

Hata hivyo, ofisi ya Wazri Mkuu Boris haikuwa tayari kuzungumiza suala hilo.

Jumatano iliyopita Umoja huo wa Ulaya ulikataa madai ya Waziri Boris kuondoa mpango wa kutokuwa na ukaguzi mpakani ili kufikia makubaliano ya Brexit.

Kwa mujibu wa EU, kiongozi huyo wa Uingereza mpaka sasa hajatoa mbadala unaoweza kufanyakazi.

Awali Boris alimwandikia Rais wa Baraza la Umoja wa Ulaya, Donald Tusk akisisitiza kwamba Uingereza haiwezi kukubali kile inachoita hatua ya kutokuwa na ukaguzi mpakani ambayo ni kinyume na demokrasia, utaratibu ambao utaweza kuepukwa kati ya Ireland ambayo ni mwanachama wa Umoja huo na Ireland ya kaskazini ambayo ni sehemu ya Uingereza.

Tangu alipoingia madarakani mwezi uliopita, Boris amekuwa akisisitiza kwamba Uingereza itajitoa kutoka Umoja huo ifikapo Oktoba 31.

Kwa sasa waziri mkuu huyo ameongeza kasi ya matayarisho kwa ajili ya kujitoa bila makubaliano hali ambayo inaelezwa kwamba inasababisha mvurugiko mkubwa wa kiuchumi.