Bosi Magereza aeleza sababu walioachiwa kufanya uhalifu

Kamishina Mkuu Jenerali Jeshi la  Magereza, Phaustine Kasike akizungumza wakati wa mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana. Kulia ni Kamishna Uwesu Ngarama. Picha na Salim Shao

Dar es Salaam. Kamishna Jenerali wa Magereza, Phaustine Kasike amesema unyanyapaa kwa wafungwa waliopata msamaha wa Rais John Magufuli unaweza kuwasababisha wakatenda makosa ili warudi tena magerezani.

Kasike ametoa kauli hiyo siku chache tangu wafungwa 5,533 kutoka kwenye magereza mbalimbali kwa msamaha wa kiongozi mkuu huyo wa nchi na baadhi kuanza kufanya uhalifu.

Wafungwa hao waliachiwa kwa msamaha wa Rais alioutangaza Desemba 9 katika maadhimisho ya Uhuru wa Tanganyika yaliyofanyika mkoani Mwanza.

Saa kadhaa baada ya kutoka gerezani Mussa Msola aliyekuwa katika gereza la Njombe alikamatwa na polisi mkoani Njombe kwa tuhuma za kuvunja nyumba ya kulala wageni mjini Makambako.

Mjini Kibaha, Mustafa Malimi aliyeachiwa kwa msamaha huo katika gereza la Ubena Chalinze juzi alikamatwa na polisi kwa tuhuma za kuiba na kumchinja ng’ombe mwenye thamani ya Sh1.2 milioni.

Akizungumza na vyombo vya habari jana jijini Dar es Salaam, Kasike aliitaka jamii kuacha unyanyapaa kwa watu hao ili nao wajisikie kama sehemu ya jamii na kwamba ni jukumu lao kuwasaidia na kuwaunga mkono katika maisha yao mapya ya uraiani.

“Ninaitaka jamii iache unyanyapaa kwa wafungwa waliosamehewa, iwapokee na kushirikiana nao ili waanze maisha mapya wakizingatia sheria za nchi. Wengine wanaathirika kisaikolojia na kuamua kufanya makosa ili tu warudi magerezani, wakiona huko ndiyo sehemu nzuri kuishi,” alisema Kasike.

Kamishna huyo alisema ni wajibu wa jamii na wadau wengine kuhakikisha kwamba walionufaika na msamaha wa Rais wanaishi kama raia wengine kwa kuwasaidia na kuwatia moyo badala ya kuwatenga.

Alisema jamii ikubali kwamba watu hao wamebadilika na wale wachache ambao bado watakuwa hawajabadilika watakumbana na mkono wa sheria kwenye maeneo yao huko huko.

Kuhusu wafungwa wanaokataa kutoka gerezani, Kasike alisema mtu anakaa gerezani akiwa na hati ya kifungo au mashauri. Alisema mfungwa huyo alinufaika na msamaha wa Rais, hivyo hakukuwa na sababu ya yeye kuendelea kukaa gerezani.

Alisema baada ya msamaha wa Rais, idadi ya wafungwa magerezani imebaki kuwa 12,665 wakati magereza yote nchini yana uwezo wa kuhifadhi wafungwa 29,902.

“Msamaha wa wafungwa umesaidia kupunguza msongamano magerezani. Pia, wafungwa wanajumuika na jamii zao na kupata fursa ya kujishughulisha na shughuli za kiuchumi,” alisema Kasike.

Kuhusu matumizi ya wafungwa kama nguvu kazi, Kasike alisema tayari wanatekeleza agizo la kuwatumia wafungwa katika shughuli mbalimbali za uzalishaji hasa kilimo na ujenzi. Alisema wametenga mashamba 10 makubwa kwa ajili ya kilimo.