Bosi Necta azungumzia walivyoshughulikia rufaa za vyeti feki

Muktasari:

  • Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania (Necta) Dk Charles Msonde amesema mpaka sasa wamehakiki watumishi 512,777 ambapo kati ya hao waliobainika kughushi vyeti ni watumishi 15,411 wakiwemo waalimu.

Dodoma. Katibu mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania (Necta) Dk Charles Msonde  amesema watumishi zaidi ya 1,000 kati ya waliobainika kughushi vyeti wengi wao walikata rufaa kwa vyeti tofauti na vilivyowasilisha na waajiri wao.

Dk Msonde ameeleza hayo leo Ijumaa Oktoba 18,2919 jijini Dodoma wakati wa kikao cha Baraza la Taifa la Chama Cha Waalimu Tanzania (CWT) kilicholenga kukutana na wadau mbalimbali ikiwamo Necta ili kujua mambo yanayohusu waalimu.

Hata hivyo, amesema watumishi zaidi ya 1,000 waliokata rufaa, wengi wao waliwasilisha vyeti vipya vyenye daraja la nne tofauti na vilivyowasilishwa awali na waajiri wao vyenye daraja la kwanza na la pili.

Amesema baada ya kuona hayo aliwaambia watumishi wake waandike kuwa watumishi hao waliowasilisha vyeti hivyo wameghushi kwani viko tofauti na vilivyowasilishwa na waajiri wao.

“Katika zoezi la uhakiki, tumelifanya kwa awamu 15 na wamehakiki watumishi 512,777 ambapo kati ya hao waliobainika kughushi vyeti ni watumishi 15,411 waliwemo waalimu.”

“Kati ya hao wengi wao waliobainika kughushi walijua na wengine pengine walisaidiwa na waajiri wao,” amesema Dk Msonde

“Kati ya hao tulihakiki watumishi 290 ni kutoka CWT kati yao 30 walibainika kughushi vyeti na kati ya hao sita walikata rufaa ambapo mmoja alibaikia kulikuwa na makosa ya namba moja katika cheti chake,” amesema

Dk Msonde akizungumzia suala la uadilifu amesema walimu wanatakiwa kuwa waadilifu katika usimamizi wa mitihani kwa maslahi ya Taifa kwani mtihani wa somo moja ukivuja Serikali inapata hasara ya Sh100 bilioni.

Aali, Rais wa CWT, Leah Ulaya amesema kwa sasa walimu wanafanya kazi kwa moyo na uadilifu tofauti na ilivyokuwa kipindi cha nyuma licha ya kuwa kuna mambo ambayo wanahitaji Serikali iyafanyie kazi ikiwa ni pamoja na upandishaji wa madaraja uende sambamba na kiwango  cha mshahara.