Bosi TFS aipigia chapuo hifadhi ya Kalambo

Kamishna Mhifadhi wa Misitu Profesa Dos Santos Silayo akiwa kwenye hifadhi ya mazingira asilia ya Kalambo

Muktasari:

Brigedia Jenerali Mkeremy awahamasisha Watanzania kutembelea hifadhi ya msitu wa Kalambo mkoani Rukwa kujionea utajiri wa maliasili

 


Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Brigedia Jenerali Mbaraka Mkeremy amesema taasisi hiyo inafanya kazi kubwa kuhakikisha inasimamia rasilimali za misitu zilizopo ili ziwe endelevu kwa kizazi cha sasa na kijacho.

Brigedia Jenerali Mkeremy ameyasema hayo akiwa kwenye Msitu wa Hifadhi ya Mazingira asili ya Kalambo mkoani Rukwa Agosti 18, 2019 ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kutembelea maeneo ya hifadhi za misitu na mashamba ya miti ya Serikali.

Alisema uamuzi wa Serikali kuupandisha hadhi msitu wa Kalambo kuwa msitu wa hifadhi ya mazingira asili ni jitihada za kuhakikisha maporomoko ya mto huo yanahifadhiwa na kusimamiwa ipasavyo.

Brigedia Jenerali Mkeremy alisema ni wakati sasa kwa Watanzania kuanza kuwa na utamaduni wa kutembelea hifadhi hiyo ili kujionea maajabu ya maporomoko hayo.

“Eneo hili linavutia na zuri kwa utalii, nitoe wito kwa Watanzania wakiwa katika siku za mapumziko na sikukuu kutembelea na kushuhudia maajabu ya maporomoko haya ambayo yameshatangazwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (Unesco) kuwa ni urithi wa dunia.”

“Niwapongeze TFS kwa ujenzi wa ngazi zenye urefu wa mita 1,277 zinazoshuka hadi kwenye maporomoko haya yanayomwaga maji ziwa Tanganyika.”

“Nimeambiwa kuwa katika ngazi za kushuka chini kwenye maji kuna “view point”  tatu  ya kwanza unapotoka kwenye maji  imepewa jina la Mheshimiwa waziri wa Maliasili na Utalii n “Kigwangala view point” napendekeza katika “view point” ya  pili  ambayo ni ya kwanza unapoteremka ngazi iitwe Dos Santos View point na ya tatu  inayofuatia iitwe, “Mkeremy view point,” alisema

Kwa upande wake, Kamishna Mhifadhi wa Misitu, Profesa Dos Santos Silayo alisema TFS imeweka mikakati kadhaa katika kuhakikisha misitu yake inaingiza mapato ya kutosha kupitia huduma za utalii sambamba na kuuza mazao ya misitu.

Profesa Silayo alisema miongoni mwa mikakati hiyo ni kuvitangaza vivutio vya utalii ekolojia vilivyopo kwenye misitu ya mazingira asilia iliyo chini ya taasisi hiyo.

“Utalii ekolojia na biashara ya mazao ya misitu na nyuki ni nguzo ya utendaji kazi wa taasisi yetu, tunafanya kila liwezekanalo kuimarisha maeneo ya Maporomoko ya Kalambo ili yaweze kutusaidia kuongeza tija katika jukumu letu la ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali, kuongeza mauzo ya nje na fedha za kigeni kupitia huduma za utalii na uuzaji wa mazao ya nyuki,” amesema Profesa Silayo