Bosi sekretarieti ya maadili amtaja Mbowe

Kiongozi wa upinzani bungeni nchini Tanzania, Freeman Mbowe

Muktasari:

Kamishina wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma nchini Tanzania, Jaji Harold Nsekela amewataka viongozi wa umma nchini humo kuhakikisha wanajaza fomu za maadili kama inavyopaswa kwa wakati pasina kulazimishwa.

Dodoma. Kiongozi wa upinzani bungeni nchini Tanzania, Freeman Mbowe ametajwa kuwa moja ya watu wanaotakiwa kuigwa katika urejeshaji wa fomu za maadili ya viongozi wa umma.

Mbowe alitajwa jana Ijumaa Desemba 6, 2019 na Kamishina wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma nchini Tanzania, Jaji Harold Nsekela katika siku ya Maadili na Haki za Binadamu ambayo ilihudhuriwa na viongozi wakuu katika taasisi zinazohusika na haki za binadamu na utawala bora.

Alisema kila tarehe ya mwisho ya Desemba huwa ni lazima kwa viongozi wa umma kutoa taarifa za madeni na mali zao jambo ambalo wengi wamekuwa wakilitekeleza kwa kusukumwa.

“Lazima taarifa hizo ziletwe na mhusika mwenyewe na si vinginevyo, kama mtu amebanwa basi atoe taarifa, tunao mfano kwa Mheshimiwa Mbowe kuna wakati alikuwa gerezani lakini mapema alituandikia barua ya kutoa taarifa ya kuchelewa kuleta kwa sababu ambayo ilikuwa na msingi, huo ni mfano mwema wa kuigwa,” alisema Jaji Nsekela.

Mbowe ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chadema pamoja na mbunge wa Bunda Mjini, Esther Matiko walikaa gerezani kwa zaidi ya siku 100 baada ya kufutiwa dhamana na Mahakama ya Kisutu jijini Dar es Salaam katika kesi iliyokuwa inawakabili.

Hata hivyo, kiongozi huyo alisema kasi ya viongozi kutoa taarifa zao ni nzuri kwani katika kipindi cha 2018 viongozi 15,303 walirejesha fomu za maadili ambao ni sawa na asilimia 98 ya viongozi 15,552 ya viongozi waliotakiwa kurejesha fomu hizo.

Alisema kwa mujibu wa sheria ni kosa kwa kiongozi kutojaza fomu za maadili kwani jambo hilo lipo kwa mujibu hivyo wanaoshindwa kurejesha, wanakuwa wamekiuka maadili.

Waziri wa nchi Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala bora nchini Tanzania, George Mkuchika alisema maadili kwa viongozi ni jambo lisilohitaji mjadala kwani Serikali imeendelea kuwa macho na kuwamulika wote ambao wanakiuka maadili.

Mkuchika alisema wameshawaonya baadhi ya viongozi na kuwafukuza ndani ya utumishi kwani kuna watu wameshindwa kushauri na badala yake wamekuwa ni watu wa kuwaweka ndani wenzao.

Alisema kuna baadhi ya watu wanashindwa kutumia nafasi zao na badala yake wamekuwa ni watu wa kuwaweka ndani viongozi wa ngazi ya chini jambo ambalo amekuwa akilipigia kelele.

“Kwa sasa tunaanza kuwashughulikia hata polisi ambao wanakubali kuweka watu ndani, hivi unawezaje kukubali kiongozi amuweke ndani mtu bila kukupa maandishi, nawaambia tutawashughulikia watoa amri na wale polisi ambao wanakurupuka na kuwaweka watu hao,” alisema Mkuchika.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria, Amos Mpanju alisema suala la watu kufukuzwa kazi bila kufuata utaratibu siyo jambo jema lakini akatetea uamuzi ambao hutolewa na Rais wa Tanzania, John Magufuli kwa kuwatumbua watu kwamba yupo sahihi.

Mpanju alisema ili mtu afukuzwe ni lazima kuwepo na sababu na nafasi ya kusikilizwa kwanza, lakini kwa kiongozi mkuu wa nchi hilo ni jambo la kawaida maana ndiyo mwenye uamuzi wa mwisho.

Kilele cha siku ya maadili imesogezwa mbele  badala ya Desemba 10, 2019 sasa itakuwa Desemba 11, 2019 ili kuwapa nafasi viongozi kutoka jijini Mwanza ambako zitafanyika shereza za miaka 58 ya Uhuru Desemba 9, 2019 na kuwa na muda wa kusafiri hadi Dodoma.