Bulaya ajitetea kortini, agusia ushauri wa wapinzani bungeni

Viongozi wa Chadema wakiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi  Kisutu katika shauri lao la ukiukwaji wa kufuata utaratibu wa kufànya mkusanyiko bila kuwa na kibali.Picha na Omar Fungo

Muktasari:

Kesi inayowakabili viongozi wa chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania cha Chadema imeendelea kwa mshtakiwa wa tisa ambaye kutoa utetezi wake akizungumzia masuala kadhaa ikiwamo ushauri ambao wabunge wa upinzani huwa wanautoa kwa Serikali ya Tanzania.

Dar es Salaam. Mshtakiwa wa tisa katika kesi inayowakabili viongozi tisa wa Chadema nchini Tanzania, Ester Bulaya ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam kuwa hajawahi kupewa taarifa na Ubalozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini kama anatafutwa na jeshi la Polisi.

Bulaya ambaye Mbunge wa Bunda Mjini (Chadema) ameeleza hayo leo Alhamisi Desemba 6, 2019 baada ya kuulizwa na wakili wa utetezi, Peter Kibatala kama aliwahi kuambiwa na ubalozi anatafutwa na Jeshi la Polisi.

Akiendelea kutoa ushahidi mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Thomas Simba, Bulaya amedai alipewa taarifa anatafutwa na Jeshi la Polisi nchini Tanzania akiwa Bunda mkoani Mara wiki moja baada ya Mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee kukamatwa.

Amedai katika shtaka la kuongoza wananchi wa Kinondoni kuandamana hakuna shahidi yoyote wa upande wa mashtaka aliyewahi kuthibitisha waliofanya maandamano ni wakazi wa Kinondoni pekee.

Akiongozwa na Wakili Kibatala aliulizwa ni kwa namna gani wabunge wanatoa mawazo yao bungeni, Bulaya amedai mawazo huwa yanatolewa lakini yanaweza yasisikilizwe kwani mawazo hayo yanatolewa uamuzi na wabunge wengi ambao ni wa chama tawala (CCM).

Bulaya ameeleza mifano ya mawazo yaliyotolewa na upinzani ni  pamoja na sheria ya mifuko ya hifadhi ya jamii kuhusu vikokotoo, sheria ya vyama vya siasa na sheria ya uhalifu wa mitandao.

Akihojiwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Saimon, Bulaya alidai unapotaka kwenda nje ya nchi ni lazima kutumia viwanja vya ndege vya Tanzania.

Amedai tofauti na ubunge, katika chama chake ni mjumbe wa kamati kuu.

Tayari washtakiwa nane kati ya tisa wameshatoa ushahidi wao katika kesi inayowakabili. Kesi hiyo imeahirishwa hadi Desemba 19, 2019 itakapoendelea kwa Bulaya kuwasilisha hati ya kusafiria.

Mbali na Mdee, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, naibu makatibu wakuu, John Mnyika (Bara) na Salum Mwalimu (Bara); Mchungaji Peter Msigwa (Iringa Mjini); John Heche(Tarime Vijijini); Ester Bulaya (Bunda) na katibu mkuu wa chama hicho, Dk Vicent Mashinji.

Washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka 13 likiwemo la kula njama, ambapo wote wanadaiwa kuwa Februari Mosi na 16, 2018 Dar es Salaam walikuĺa njama ya kutenda kosa la kufanya mkusanyiko usio halali na kukiuka amri ya jeshi la polisi ya kutawanyika.