Bunge Tanzania laanzisha kwaya, Spika Ndugai atoa neno

Kikundi cha Kwaya cha Bunge kikiimba wimbo wa Taifa pamoja na wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wakati wa kuanza kwa kikao cha kwanza cha mkutano wa 18, jijini Dodoma leo asubuhi. Picha na Edwin Mjwahuzi

Muktasari:

Mkutano wa 18 wa Bunge, kikao cha kwanza kimeanza leo Jumanne Januari 28, 2020 na kitahitimishwa Februari 7, 2020.

Dodoma. Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai ameipongeza kwaya ya Bunge ambayo leo Jumanne Januari 28, 2020, imeimba vizuri wimbo wa Taifa na wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wakati wa ufunguzi wa mkutano wa 18 kikao cha kwanza cha Bunge la 11.

Awali, wimbo wa Taifa na ule wa Afrika Mashariki wakati wa ufunguzi na ufungaji wa mikutano ya Bunge ulikuwa ukiimbwa na kwaya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), lakini leo uliimbwa na watumishi wa Bunge.

Watumishi hao waliovaa majoho waliimba wimbo wa Taifa na ule wa  Afrika Mashariki.

Baada ya kumaliza kuimba na dua ya kuliombea Bunge na Taifa, Spika Ndugai amesema hatua hiyo ya kwaya kuimba wimbo huo inatokana na uamuzi wa Kamati ya Uongozi ya Bunge uliotolewa Januari 2020.

Amelishukuru Jeshi la Polisi Tanzania kwa kuwafundisha watumishi hao ambapo baada ya kuimba wabunge waliwapigia makofi kuwapongeza.

 

Endelea kufuatilia Mwananchi kujua kinachoendelea bungeni